Na Tabitha Joshua, CHANG’OMBE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imeanzisha programu iitwayo TAKUKURU Rafiki inayolenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika kukabili vitendo vya rushwa kwa jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Michael Sanga katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Chang’ombe iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Sanga alisema “TAKUKURU Rafiki ipo kwa lengo la kufikia wananchi kwa karibu na kutatua kero zao wenyewe ambazo zinapatikana katika idara zote, zinazopatikana katika kata hii. Vikao vyote vinavyohusu TAKUKURU Rafiki vinafanywa katika ngazi ya kata Mwenyekiti wake ni diwani wa kata na katibu wake anakuwa ni Afisa Mtendaji wa Kata”.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Tunu Dachi aliishukuru Ofisi ya TAKUKURU kwa kuanzisha proramu hii kwasababu imeweza kuondoa kero za wananchi katika kata hii. “Katika kikao hiki, tumeweza kupata kero mbalimbali takribani kero tisa katika idara tofauti. Kero hizo zilihusu maji, kero za vijana wa bodaboda, ubovu wa miundombinu katika soko kipindi cha mvua na barabara, na pia tumehakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja kero walizozitoa zitakuwa zimepewa majibu” alisema Dachi.
Alisema kuwa katika kikao hicho, kamati ndogo imechaguliwa ambayo ina mwenyekiti, katibu na mtendaji kwa lengo la kuharakisha kushugulikia na kutatua kero za wananchi.
Mwenyekiti aliyeteuliwa katika kamati ndogo, Jafari Musa Athumani alisema kuwa amefurahishwa na juhudi za TAKUKURU Rafiki kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na kutatua kero za wananchi. “Ni vizuri kwa TAKUKURU jinsi walivyotoa elimu kwasababu watu wengi hawaelewi juu ya jambo hilo na pia ni vizuri kuwa watu wametoa kero zao ili ziweze kushughulikiwa” alisema Mwenyekiti Athumani.
Mwenyekiti huyo aliwataka wananchi kutokuwaogopa TAKUKURU badala yake badala yake kuwapa ushirikiano mkubwa kwa kutoa taarifa za vitendo cha rushwa katika Kata. “Kwa hatua hii taifa litafika mbali kwasababu itakuwa imeweza kutatua yale matatizo ambayo yameweza kuharibu uhusiano kwenye jamii nzima” alisema Athumani.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wafanyabiashara, wananchi, viongozi wa dini, wanasiasa, viongozi wa serikali za mitaa, Chama Cha Mapinduzi na wadau mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.