WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo ameiagiza timu ya wataalamu wa ufuatiliaji wa fedha za miradi kutoka ofisi hiyo kufanya uchunguzi na ukaguzi wa kina wa Sh bilioni 1.2/- zilizotumika kununua vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ikiwamo ujenzi wa majengo ya hospitali ya wilaya, Waziri Jafo alisema timu hiyo ya wataalamu itaanza kazi yake muda wowote kuanzia leo (juzi) kubaini kama fedha hizo zimetumika kununulia vifaa vya ujenzi wa hospitali au la.
Amesema wataalam hao watafuatilia ununuzi wa vifaa vya ujenzi uliofanyika katika ujenzi wa hospitali hiyo ili kuhakikisha matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali yanaendana na majengo yaliyojengwa.
“Nimekuja hapa nikiwa na taarifa kuwa fedha zilizotolewa na Rais (John Magufuli) kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, Sh bilioni 1.2 zimeliwa. Leo (juzi) nilikuja ili kuondoka na kichwa cha Mkurugenzi, na maamuzi haya nilipaswa niyafanye tangu sijaja hapa.
Alisema endapo itabainika kuna makosa yalifanyika, hatua zitachukuliwa baada ya kujiridhisha kuwa kweli taarifa ya awali inaonesha fedha hizo zimeliwa na ofisi ya Halmashauri ya Malinyi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika alisema utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na wao kukosa umakini na utekelezaji wake unafanyika kwa siri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Mussa Mnyeti alimweleza Waziri Jafo kuwa Sh bilioni 1.2 zimenunulia vifaa vya ujenzi wa hospitali na Sh milioni 220 zimebaki na zitatumika kwenye umaliziaji.
Chanzo: Tovuti ya HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.