WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kujipanga na kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa ardhi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utendaji kazi na usimamizi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri.
Dkt. Mabula alisema hayo leo Oktoba 1, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo mji wa Serikali Mtumba. Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupata maoni juu ya muundo mpya wa utendaji kazi wa wataalam wa ardhi katika ngazi ya Halmashauri.
Dkt. Mabula alisema, zimeanza kujitokeza changamoto katika utendaji kazi kati ya watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa Halmashauri hasa katika eneo la usimamizi wa sekta hiyo baada ya kuanza utekelezaji wa rejesho la Waraka wa Utumishi Na. 1 wa Mwaka 1998 kuhusu usimamizi wa watumishi wa sekta ya ardhi na maji kutokana na sababu mbalimbali.
Rejesho hilo pamoja na mambo mengine liliwahamisha wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka kwenye usimamizi wa Mamlaka za serikali za mitaa kiajira na kinidhamu na kuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi.
''Watumishi hawa kiajira na kinidhamu wako Wizara ya ardhi mamlaka za upangaji ardhi ziko Halmashauri lakini baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakijiweka mbali na wataalam wa ardhi na kushindwa kufuatilia utekelezaji wa sekta ya ardhi au kukosa ufahamu katika sekta ya ardhi.'' Alisisitiza Dkt. Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula changamoto hiyo imeleta mkanganyiko kwa kuwa baadhi ya watendaji hasa wakurugenzi hawaoni kama wanawajibu wa kusimamia sekta ya ardhi wakati wao ni mamlaka za upangaji ardhi.
Chanzo: wizara_ya_ardhi (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.