MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amepewa zawadi ya cheti na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufuatia ubunifu wake wa kuanzisha program ya kufundisha wanafunzi kwa njia ya redio za Dodoma na mitandao ya kijamii katika mapumziko ya Covid-19.
Zawadi hiyo ya cheti imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Selemani Jafo katika siku ya TAMISEMI, maalum kwa sekta ya elimu iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma leo.
Akitoa maelezo mafupi ya utangulizi kuhusu zawadi hivyo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli amesema kuwa vyeti hivyo vinatolewa kwa watumishi waliofanya vizuri katika mapambano ya Covid-19 katika sekta ya elimu.
Vyeti hivi ni maalum kwa walimu wa Jiji la Dodoma kwa sababu wakati nchi inaendesha program ya kufundisha wanafunzi katika televisheni kitaifa, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi aliamua kuanzisha program yake katika redio za ndani ya Jiji la Dodoma kwa kutumia walimu wake. Hivyo, tukaona ni vema kuwatambua hii ni kutokana na maelekezo yako wewe mwenyewe mheshimiwa Waziri kuwa tuwatambue wale wote walioshiriki katika kufundisha wanafunzi wakati wa likizo ya Covid-19. Hivyo, hii ni zawadi maalum kwa Mkurugenzi wa Jiji na walimu wake” amesema Mweli.
Wengine waliopata zawadi za vyeti ni Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mabeyo, Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Upendo Rweyemamu na walimu wote walishiriki kufundisha vipindi katika redio za Jiji la Dodoma.
Akiongelea zawadi ya cheti hicho, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliyepokea cheti hicho, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Sharifa Nabalang’anya amesema kuwa cheti hicho ni heshima kubwa kwa Halmashauri. “Mkurugenzi amepatiwa cheti hicho kwa kutambua juhudi za utoaji elimu kwa wanafunzi wakati wa mapambano ya Covid-19. Jiji liliona ni muhimu kwa wanafunzi kupata elimu kupitia redio na mitandao ya kijamii badala ya kubaki nyumbani. Cheti hiki ni heshima kubwa kwa Mkurugenzi wa Jiji na Halmashauri kwa ujumla” amesema Nabalang’anya.
Siku maalum ya TAMISEMI (TAMISEMI Day) kuhusu sekta ya elimu inalenga kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo na imehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo.
Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Seleman Jafo (wa tatu kulia) akimkabidhi Sharifa Nabalang'anya aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kupokea cheti cha kutambua mchango wake wa kutoa elimu kwa wanafunzi wakati likizo ya mapumziko wakati wa mapambano ya Corona. Kulia kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga.
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Upendo Rweyemamu (kushoto) akiwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Joseph Mabeyo wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma waliposhiriki kwenye Siku ya TAMISEMI (Sekta ya Elimu) ambapo walikuwa miongoni mwa waliotunukiwa Cheti kutambua mchango wao wa kutoa elimu wakati wa likizo ya Corona.
Baadhi ya walimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma walioshiriki kutoa elimu kwa njia ya redio na mitandao ya kijamii wakati wa likizo ya Covid-19 ambao nao OR-TAMISEMI imewapa cheti kutambua mchango wao kwa jamii katika kutoa elimu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.