MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amewataka wataalamu wa Wakala wa barabara nchini TANROADS Mkoa wa Dodoma na Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA kujenga utaratibu wa kuwa karibu na wakandarasi waliopewa miradi katika maeneo yao ili miradi hiyo itekelezwe kwa viwango na kwa wakati.
Dkt Mahenge ametoa maagizo hayo Machi 17, 2021 jijini Dodoma wakati wa kikao cha bodi ya barabara Mkoa wa Dodoma waliokutana kutathmini utekelezaji wa bajeti na namna ya kuboresha bajeti mpya 2021 hadi 2022 amesema kila taasisi katika eneo ambayo mkandarasi amesaini mkataba asimamiwe kikamilifu.
“Mimi nimepita katika miradi hiyo nimeona wakandarasi wapo site (eneo la kazi) na maeneo mengi wametengeneza lakini mvua zimeharibu na ukizingatia serikali imeshatoa fedha hakuna fedha nyingine mkandarasi asimamiwe akarabati kwenye uharibifu” amesema Dkt Mahenge.
Amesema taasisi hizo ni muhimu sana katika kuunganisha Mikoa, Wilaya, Vijiji na mitaa hivyo ni vyema viongozi wa taasisi hizo kufanyakazi kwa weredi kuhakikisha wananchi wanaunganishwa na mawasiliano ya barabara ili kujikwamua kiuchumi.
Aidha ameitaka TARURA kujenga utaratibu wa kutembelea halmashauri husika kabla ya kutenga bajeti au kuainisha barabara za kukarabati ili wapate mahitaji halisi kutoa kwenye halmashauri husika na uhitaji na umuhimu wa barabara kabla ya kuzitengea bajeti barabara hizo.
“TARURA muende kwenye halmashauri husika huko mtajua mahitaji halisi ya halmashauri hizo wao watawaambia bara bara ipi ni muhimu sana kwa kipindi hicho kuliko ninyi kupanga tu bajeti bila kujua sehemu zenye mahitaji sana” amesema.
Ametaka ahadi zote za viongozi wa kitaifa ziainishwe kwa Pamoja na zipewe kipaombele na msukumo ili fedha hizo ziweze kutengwa ili ahadi hizo zitimizwe, huku akiwataka viongozi wa ngazi zote katika halmashauri za Mkoa wa Dodoma kuwa wasimamizi wa miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara nchini TANROADS Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda akieleza utekelezaji wa miradi ya TANROADS amesema kwa mwaka wa fedha 2019 – 2020 walitengewa zaidi ya bilioni 18 kwa matengenezo na ukarabati wa barabara mbalimbali.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2020 na 2021 pia walitengewa zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa matengezezo ya barabara kuu na barabara za Mkoa huku ikiwa imesaini jumla ya miradi 37 ya barabara ikiwa na ujenzi wa madaraja makubwa mbalimbali.
Nae mratibu wa RARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe amesema TARURA inajumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 6996.25 kati ya hizo barabara 2695.75 barabara za mikusanyiko, 3403 barabara za mlisho na barabara 897 ni barabara za kijamii.
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu tawala Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy amesema ni vyema wajumbe wa kikao hicho kushiriki katika vikao vya ngazi ya chini kwenye maeneo yao ili kubainisha changamoto na makubaliano tangu ngazi za chini katika maeneo wanayotoka.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.