SERIKALI kwa kushirikiana na wadau inaandaa Tamasha Maalum la kuelimisha Jamii kuhusu fursa za maendeleo ya kiuchumi, linalojulikana kama ‘Tanzania Development Festival (TDF).
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akitambulisha Tamasha hilo katika mkutano na vyombo vya Habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam alisema Tamasha hilo litakalokuwa na Kaulimbiu isemayo "Zijue Fursa, Imarisha Uchumi, Kataa Ukatili, Kazi Iendelee (ZIFIUKUKI)" litasaidia kuwapatia wananchi huduma stahiki sambamba na kutoa elimu ya kupambana kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto.
Dkt. Gwajima amebainisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kufanya juhudi kuhakikisha wananchi wanapata elimu na ufahamu wa fursa za maendeleo hivyo, kwa kuzingatia mwitikio wa wadau, Wizara imeona umuhimu wa kuwa na Jukwaa la pamoja la Wadau wote wa Maendeleo ili kuunganisha nguvu ya kuhamasisha mwamko wa jamii kutambua fursa za kiuchumi.
Ameongeza kuwa pamoja na kutambua fursa hizo, Jamii itahamasishana kukataa ukatili wa kijinsia na kwa watoto na kupata uelewa wa mifumo inayojielekeza kwenye kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwani ukatili ni adui wa maendeleo na ustawi wa jamii.
"Ufuatiliaji unaonesha baadhi ya wananchi hasa wanawake, wajane, wazee na wengine wenye mahitaji maalumu elimu haijawafikia kikamilifu. Kupitia tamasha hili sehemu kubwa ya jamii itazidi kuelimika na kufahamu kuhusu; uwepo wa mikopo bila riba kwa makundi maalumu, huduma za mikopo ya benki mbalimbali kwa riba nafuu" alisema Gwajima.
Ameongeza pia lengo la Tamasha hili litakalozinduliwa tarehe 27 hadi 29 Aprili, 2023 katika viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam ni kuifikia jamii kwa elimu na huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo kutoka Sekta Binafsi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.