WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema tatizo la ongezeko la bei la mazao kadhaa ni la muda, kwani hadi sasa nchi ina akiba ya chakula cha kutosha cha tani 53,000 katika kipindi cha mwaka 2019.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa kuhusu Hali ya Uchumi kwa mwaka 2019, Dk Mpango alisema ongezeko la bei za bidhaa za vyakula, linategemewa kuwa la muda mfupi, kwani bado nchi inayo akiba ya kutosha ya chakula.
Alisema katika kipindi hicho, pia mfumuko wa bei wa chakula, uliongezeka kufikia wastani wa asilimia 6.7 Novemba 2019, ikilinganishwa na asilimia 2.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.
Dk Mpango alisema ongezeko hilo, lilitokana na changamoto za usafirishaji, miundombinu ya masoko, maghala na ugavi wa bidhaa za vyakula kimaeneo. Alisema uhaba wa vyakula kwa nchi za jirani, ulisababisha soko la vyakula kwa nchi hizo kuwa kubwa na kuvutia wafanyabiashara nchini, kusafirisha bidhaa za chakula na kuziuza katika nchi hizo.
Dk Mpango alisema mfumuko wa bei, uliendelea kubakia ndani ya lengo la asilimia 5.0 katika mwaka ulioishia Novemba 2019. “Katika kipindi hicho, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 ukilinganishwa na asilimia 3.0 katika kipindi kama hicho 2018. Kiwango hiki ni chini ya lengo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki la asilimia 8,” alisema.
Alisema nchi nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nazo zilikuwa na viwango vidogo vya mfumuko wa bei. Dk Mpango alisema mfumuko wa bei katika kipindi kilichoishia Novemba 2019, kwa Kenya ni asilimia 5.6 na Uganda ilikuwa asilimia 3.
Alisema mfumuko wa bei wa chakula uliongezeka Novemba 2019, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018 na ulitokana na changamoto za usafirishaji. “Ongezeko hili lilitokana na changamoto za usafirishaji, miundombinu ya masoko, maghala na ugavi wa bidhaa za vyakula kimaeneo,” alisema.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.