Bunge jana lilikubali kuunda mbuga tatu za kitaifa, na kufanya idadi ya mbuga nchini kufikia 24 ambayo ni idadi ya juu zaidi barani Afrika.
Akizungumza baada ya kuidhinishwa kwa mpango huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla aliielezea hatua hiyo kama hatua muhimu katika azma ya Tanzania ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kila mwaka.
Hifadhi mpya za kitaifa zinatokana na kupandishwa hadhi kwa pori la akiba la sasa la Kigosi katika Mkoa wa Kigoma na pia pori la akiba Ugalla lililopo karibu na Mkoa wa Tabora.
Hifadhi hizo tatu zitaongeza idadi ya mbuga za kitaifa kutoka mbuga 19 za ardhi zinazosimamiwa sasa na Hifadhi za Kitaifa za Tanzania (TANAPA) hadi kufikia 22 pamoja na mbuga mbili mbili za baharini ambazo ni Hifadhi ya Marine Island kwenye ukanda wa pwani na Mnazi Bay-Ruvuma Estuary Marine Park.
"Kwa hesabu ya mbuga hizo 24 za kitaifa nchi yetu itaongoza bara la Afrika kwa idadi kubwa zaidi ya hifadhi za kitaifa, ikiipita Kenya ambayo ina hifadhi 23" alisema Dk Kigwangalla.
Waziri huyo alionyesha matumaini kwamba kwa kuongoza katika idadi ya mbuga za kitaifa, Tanzania itakuwa kwenye nafasi nzuri kuliko ilivyokuwa hapo awali katika juhudi zake za kuongeza utalii wa kimataifa pamoja na kupata fedha nyingi za kigeni zinazohitajika sana kukuza uchumi wetu.
"Hii inatupa fursa katika kuitangaza nchi kama sehemu yenye idadi kubwa ya vivutio vya utalii" alisema.
Hata hivyo, wakichangia hapo awali, baadhi ya Wabunge walitahadharisha kwamba kuna maswala ambayo yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi kabla ya kuendelea na mpango huo.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mwenyekiti Kemilembe Lwota alisema kwamba ili kuhakikisha tunazuia mizozo kuhusu mbuga mpya za kitaifa, serikali inapaswa kufanya kazi na jamii zinazoishi ndani au karibu na maeneo yaliyotengwa ili kuhakiki mipaka.
"Kuna vijiji vinavyotambuliwa kisheria ndani ya mbuga. Kuna watu wengi wanaojihusisha na shughuli za ufugaji wa nyuki ndani ya mbuga zote mbili na pia idadi kubwa ya watu ambao maisha yao yanategemea uvuvi kwenye Mto Ugalla" alisema Lwota.
Mnamo mwezi Julai, Rais John Magufuli alitoa agizo la kuanzishwa kwa Hifadhi ya Kitaifa ya Nyerere, ambayo itamegwa katika sehemu ya juu ya Hifadhi ya Mbuga ya Selous.
Kabla ya agizo hilo, Rais alikuwa aliagiza Hifadhi ya Kitaifa ya Burigi-Chato ambayo ilipandishwa kutoka hadhi ya pori la akiba.
Chanzo: Gazeti la The Guardian (www.ippmedia.com)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.