Timu ya Taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) ‘Tanzanite Queens’ imeibuka bingwa wa mashindano ya soka ya wanawake ya Nchi za Kusini mwa bara la Afrika (COSAFA) baada ya kuifunga timu ngumu ya Taifa ya Zambia 4-3 kwa mikwaju ya penalti.
Timu ya wanawake ya Tanzania (U-17) ilionesha kabumbu safi katika mchezo huo uliochezwa katika dimba la Nelson Mandela Bay nchini Afrika ya Kusini.
Zambia ndiyo walitangulia kupata goli kupitia mshambuliaji wao Comfort Seleman dakika ya 19 baada ya kutumia vizuri makosa ya walinzi wa Tanzania, na kumuinamisha nyavuni golikipa Aisha Mrisho. Hadi kipindi cha kwanza kinaisha Zambia ilikuwa mbele kwa goli 1.
Kipindi cha pili kilianza kwa Tanzania kuonesha kandanda safi na kusawazisha goli hilo kwa mkwaju wa penalti kufuatia Aisha Masaka kuchezewa madhambi ndani ya 18, na Koku Kipanga kufunga penalti hiyo na kufanya dakika 90 kuisha kwa goli 1-1.
Katika mikwaju ya penalti wanawake wa Tanzania waliibuka kidedea baada ya kufunga penalti 4 dhidi ya 3 walizopata wanawake wa Zambia.
Itakumbukwa kuwa Timu ya Tanzania U-17 ilitinga fainali kibabe baada ya kushinda dhidi ya Comoro (5-1), kufungwa na Zambia (0-1), kuifunga Afrika Kusini (6-1) kabla ya kuisambaratisha Zimbabwe (10-1). Aidha, timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini siku ya Jumatatu saa 7:15 usiku.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.