WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema kiasi cha Bilion 71.7 za Kitanzania zitatumika kuiunganisha Uganda na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kipindi cha miaka 15.
Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa Hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya Kibiashara ya Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Uganda (NBI) iliyofanyika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, leo Septemba 29, 2023.
“Leo hii tumeshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano – NICTBB na Mkongo wa Mawasiliano wa Uganda. Mkataba huu una thamani ya kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 28 sawa na fedha za Kitanzania Shilingi Bilion 71.7 kwa kipindi cha miaka 15. Mikongo hii itaunganishwa kupitia mpaka wa Tanzania na Uganda, eneo la Mutukula katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.” Amesema Waziri Nape.
“Ni matumaini yetu, kuona Afrika ya Kidigitali (Africa Digital) inafikiwa na matokeo yake chanya yanasaidia katika kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na shughuli za kijamii barani Afrika kwa kutumia teknolojia. Ni matumani yetu kuona Afrika yenye mifumo imara ya Serikali Mtandao, Elimu Mtandao, Afya Mtandao, Biashara Mtandao, Kilimo Mtandao katika kutoa huduma kwa wananchi wetu.” Amesema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kusimamia vyema kutoa huduma kwa mujibu masharti yaliyopo kwenye mkataba wa makubaliano.
“Tuhakikishe tunatoa huduma bora na yenye uhakika, panapotokea changamoto yoyote ile iweze kushughulikiwa kwa haraka. Uganda inategemea huduma bora kutoka kwenu, mkatoe huduma yenye ubora kwa kuzingatia makubaliano ya Waheshimiwa Ma-Rais wetu. Kwa changamoto ambazo zitakuwa nje ya uwezo wenu, mziwasilishe Wizarani kupata ufumbuzi wa haraka”. Amesisitiza Waziri Nape.
Katika hatua nyingine, Waziri Nape amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania, Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Peter Ulanga na Dkt. Hatwib Mugasa Mkurugenzi Mtendaji wa NITA-U kwa kubeba jambo hili kwa uzito wake na kufanikisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Tanzania –NICTBB na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Uganda unaosimamiwa na NITA-U.
Mkataba huo umekuja mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi nchini Uganda, ambapo yeye na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoel Kaguta Museveni walikubaliana kuunganisha miundombinu mikuu ya mawasiliano ili kuiwezesha Uganda na nchi jirani kupata huduma za intaneti zenye ubora na bei nafuu na pia kuunganisha nchi ya Uganda na mikongo ya baharini iliyopo Tanzania.
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (kushoto), Mhandisi Peter Ulanga akiwa pamoja na Dkt. Hatwib Mugasa, Mkurugenzi Mtendaji wa NITA-U wakisaini Makubaliano ya Kibiashara ya Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Uganda (NBI) hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, leo Septemba 29, 2023.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.