NAIBU Waziri, Ofisini ya Rais, TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, alisema Serikali imeweza kujenga na kuimarisha miundombinu ya afya msingi, kuajiri Watumishi na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya ya Msingi.
Alisema hadi kufikia Februari mwaka 2024, Sekta ya afya ya msingi nchini Tanzania ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 6,933 zikiwamo Zahanati 5,887 Vituo vya afya 874 na Hospitali za Halmashauri 172.
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba kuna ongezeko kubwa la vituo katika Afya ya msingi ikilinganishwa na idadi ya vituo 5,270 katika mwaka 2015. Hii ni hatua kubwa katika kuelekea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote nchini Tanzania, »alisema.
Alisema kwa mwaka, 2023, wateja milioni 26.9, walipata huduma katika vituo vya afya ya Msingi kama wagonjwa wa nje yaani (OPD), wateja 854,318 walipata huduma ya kulazwa (IPD). Katika eneo la mama na Mtoto wateja milioni 1.6 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na akinamama waliokuwa na uzazi pingamizi wakafanyiwa upasuaji walikuwa ni 125,318.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuongeza idadi ya vituo vya afya ya msingi, alisema kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa kada mbalimbali za afya, Ustawi wa Jamii na Lishe na vifaa tiba mbalimbali. Upungufu huu wa watumishi, unaokadiriwa kufikia asilimia 52, na hii imetokana na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya afya ya msingi. Hii inaathiri moja kwa moja utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wetu.
Alimuomba Rais kuendelea kutoa kibali cha ajira kwa watumishi wa kada za mbalimbali za afya, Ustawi wa Jamii, na Lishe huku akiomba mashirika ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo, na Sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika eneo hilo muhimu ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.