RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuendelea kurekodi kipindi maalum cha Royal Tour kitakachotangaza utalii, biashara na uwekezaji nchini.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais alilakiwa na viongozi mbalimbali.
Akiwa njiani kuelekea Marangu, Rais alipata nafasi ya kusalimiana na wananchi wa Mererani Mkoani Manyara, Bomang'ombe Wilaya ya Hai na Himo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo aliongelea masuala mengi ya maendeleo na jitihada za Serikali anayoiongoza inavyofanya na ilivyojipanga kuhakikisha huduma za jamii zinazidi kuboreshwa.
Aidha, Mhe. Rais Samia aliongea kuhusu madini na kusema "Haya madini yana mwisho, kwa hiyo inabidi tuyachimbe kwa mpangilio maalum. Tukiyachimba ovyo ovyo tutashusha thamani ta Tanzanite yetu, tukiyauza kwa mpangilio Tanzanite yetu itapanda thamani.
Huko nyuma Tanzanite yetu ilikuwa inazagaa tu, ukienda Kenya kuna Tanzanite, sijui Singapore Tanzanite, India inauza tu ovyo ovyo. Sasa tunataka tuwaambie ulimwengu kuwa Tanzanite kwao ni hapa (Tanzania)."
Akiongelea kuhusu Royal Tour Rais amesema "Tupo na Wazungu wamekuja, tunakwenda kuchukua kama filamu ndani ya migodi yetu huku, lengo ni kuwaonesha Dunia kwamba madini ya Tanzanite kwao ni Tanzania, na tunakwenda kuwaonesha ushahidi kwamba hapa ndipo machimbo yalipo" amefafanua zaidi Rais Samia.
Tovuti ya Halmashuri ya Jiji la Dodoma inamtakia kila la heri na mafanikio mema Mheshimiwa Rais wetu katika mpango huu wa Royal Tour.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.