YALIYOJIRI LEO WAKATI MTENDAJI MKUU WA WAKALA YA BARABARA ZA VIJIJINI NA MIJINI (TARURA), MHANDISI VICTOR SEFF AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU WA WAKALA HIYO NA MWELEKEO WAKE KATIKA MWAKA WA FEDHA 2023/24
JUKUMU kubwa la TARURA ni kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya. Serikali ya Awamu ya Sita imeiongezea TARURA bajeti yake mara tatu zaidi ikiwa ni kuendeleza juhudi za Awamu zilizopita za kuboresha barabara za vijini.
Kwa sasa TARURA ipo kwenye utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Pili toka kuanzishwa kwake mwaka 2017 ikiwa na lengo kuwa, ifikapo mwaka 2025 angalau asilimia 85 ya barabara za Wilaya ziwe zinapitika kwa misimu yote.
Lengo hilo linaakisi kaulimbiu ya TARURA Mpango Mkakati wa Pili inayosema "TARURA tunakufungulia barabara kufika kusikofikika."
Mtandao wa barabara za Wilaya chini ya TARURA una jumla ya kilomita 144,429.77, kati ya urefu wa mtandao wa barabara hizo, kilomita 3,053.26 (2.11%) ni barabara za lami, kilomita 38,141.21 (26.41%) ni barabara za Changarawe na kilomita 103,235.30 (71.48%) ni barabara za udongo.
Kuna jumla ya madaraja 3,105 na makalavati 75,620 ambapo hali ya mtandao wa barabara za Wilaya hadi kufikia Juni 2023, asilimia 30.31 (km 43,773.95) una hali nzuri, asilimia 32.47 (km 46,889.14) una hali ya wastani na asilimia 37.23 (km 53,766.68) una hali mbaya.
MAENEO YA KIPAUMBELE YA TARURA
Kuzitunza barabara zilizo katika hali nzuri na hali ya wastani kubaki katika hali hiyo ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika na kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili angalau
ziweze kupitika misimu yote.
Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.
Kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa za Changarawe/Lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii. Mipango ya muda mrefu ya Kitaifa na Kimataifa, ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji.
UTEKELEZAJI WA TARURA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23
Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Wakala ilidhinishiwa jumla ya shilingi 838,158,970,993 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya, kati ya fedha hizo, shilingi
776,628,938,748 ni fedha za ndani na shilingi 61,530,032,245.58 ni fedha za nje.
Utekelezaji wa kazi za ujenzi na matengenezo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 hadi kufikia mwezi Juni 2023, umefikia asilimia 85 ambapo jumla ya shilingi bilioni 743.405 zilipokelewa sawa na asilimia 89 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 598.81 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 144.593 ni fedha za nje.
Kupitia fedha za ndani, jumla ya kilomita 22,523.51 zimefanyiwa matengenezo (utunzaji wa barabara), ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 249.74, ujenzi wa barabara kwa changarawe kilomita 9,761.01, ujenzi wa madaraja na makalavati 463 pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuondoa maji barabarani kilomita 64.47.
Kupitia fedha za nje, kulikuwa na miradi minne inayoendelea na utekelezaji ambayo ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mradi wa Uboreshaji wa Barabara vijini na fursa za kiuchumi na kijamii (RISE), Mradi wa uendelezaji wa Miji 45 (TACTIC) na Mradi wa Agri connect.
Katika mradi wa DMDP ambao umekamilika Januari 2023, kazi zilizofanyika ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami km 5.3 na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua kilomita 1.8 pamoja na maandalizi ya mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.
Katika Mradi wa Rise, mikataba miwili ya ujenzi wa km 33 za barabara kwa kiwango cha lami
ilisainiwa tarehe 20 Juni 2023 na sasa Wakandarasi wanajitayarisha kupeleka vifaa na watumishi maeneo ya kazi. Barabara zinazojengwa ni Wenda - Mgama km 19 katika Wilaya ya Iringa na barabara ya Mtili - Ifwagi km 14 katika Wilaya ya Mufindi.
Katika mradi wa TACTIC, ununuzi wa Wakandarasi na Wataalam Washauri wa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya vipaumbele katika Halmashauri za miji 12 ya kundi la kwanza (Tier 1) uko katika hatua za mwisho na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Septemba 2023.
Ununuzi wa Wataalam Washauri kwa ajili ya usanifu wa miundombinu ya vipaumbele katika miji 15 ya kundi la pili (Tier 2) umeanza kwa kutangaza zabuni tarehe 16/06/2023. Baada ya kupata Wataalam Washauri malengo ni kuanza usanifu mwezi Novemba 2023.
Utambuzi wa miradi kwa ajili ya kundi la tatu (Tier 3) ili kuandaa hadidu za rejea kwa ajili ya usanifu umeanza wiki ya mwisho ya mwezi Juni 2023. Kazi hii itafanyika sambamba na uandaaji wa mpango kabambe wa uendelezaji miji (Planning scheme).
Ununuzi wa wataalam washauri kwa ajili ya usanifu miundombinu ya vipaumbele katika miji 18 ya kundi la tatu (Tier 3) unatarajia kuanza kwa kutangaza zabuni mwezi Januari 2024.
Mikataba yote sita ya mradi wa Agri connect awamu ya pili (Tranche l) yenye thamani ya shilingi bilioni 32.1 imeshasainiwa na Wakandarasi wameshapeleka vifaa vya ujenzi eneo la kazi na kazi zimeanza katika Wilaya za Kilolo km 1.1, Wanging'ombe km 19.3, Busokelo km 6.41, Mbozi km 11.01 na Rungwe km 11.35.
Taratibu za ununuzi wa Wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi awamu ya tatu (Tranche lIl) zinatarajia kuanza mwezi Septemba 2023 baada ya kazi ya usanifu kukamilika.
MPANGO NA UTEKELEZAJI WA KAZI ZA UJENZI NA MATENGENEZO YA MIUNDOMBINU YA BARABARA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24
Katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya barabara zenye urefu wa km 21,057.06 zitafanyiwa matengenezo, km 427 zitajengwa kwa kiwango cha lami, km 8,775.62 zitajengwa kwa kiwango cha changarawe, madaraja na makalavati 855 yatajengwa pamoja na mifereji ya mvua km 70.
Jumla ya shilingi bilioni 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 710.31 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.
Mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi. Hadi Mwezi Machi, 2023 TARURA imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya shilingi bilioni 8.7 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Morogoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15.
Tunaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine ya mbali. Teknolojia hizo ni pamoja na ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer.
Hadi sasa kwa kutumia teknolojia ya ECOROADS, katika Jiji la Dodoma imejengwa km 1 ambayo imekamilika na katika Wilaya ya Mufindi zitajengwa km 10 na Mkandarasi yuko kwenye matayarisho ya kuanza kazi.
Aliyosema Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa
Watanzania tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinazofanya biashara na zisizofanya biashara zinafanya kazi zake kwa tija.
TARURA imeanzishwa mwaka 2017 lengo likiwa ni kupanua mawanda ya namna ambavyo tutawahudumia Watanzania kwa kuwaboreshea barabara.
Chanzo: IDARA YA HABARI - MAELEZO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.