Shule ya Sekondari Mpunguzi iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, imekabidhiwa msaada wa Meza na Viti 36 kutoka kwa kikundi cha kijamii kinachoitwa Tanzania Social Development Association (TASODA) maarufu kama 'Twende na Magufuli' wenye lengo la kusaidia upungufu wa madawati shuleni hapo na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kukuza sekta ya Elimu Nchini.
Akikabidhi samani hizo Naibu Katibu wa kikundi hicho Mwalimu Fredy Nyandoro amesema kuwa kumekua na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma wakiwa wamekaa chini kwa kukosa meza na viti vya kukalia hivyo wao kama kikundi wameona wajitokeze na kutoa kidogo walichonacho ili kuzikomboa shule zenye uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo.
“Lengo kuu la kikundi chetu ni kuhakikisha tunasaidia Jamii inayotuzunguka ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wetu mpendwa tumeanza na sekta Elimu lakini tutahakikisha tunagusa katika nyanja zote kama muongozo wa kikundi chetu unavyosema” Alisema Nyandoro.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mwalimu Josephat Maganga amesema kuwa kwa niaba ya Serikali ya Wilaya wanakishukuru kikundi hicho kwa kujitoa kwao kutatua kwa sehemu changamoto ya vifaa vya kukalia na kusomea shuleni hapo kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia shule hiyo kukua kitaaluma.
Mwalimu Maganga alisisitiza kuwa changamoto ya madawati mashuleni kwa sehemu kubwa inatokana na kufunguliwa kwa sekta ya Elimu hasa katika awamu hii ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutangaza elimu bure nchi nzima jambo ambalo limechangia idadi ya wanafunzi kuongezeka mashuleni.
“Sera ya Elimu bure imesaidia sana watoto wengi kuingiza shule kwani hapo awali walikua wanashindwa kwa sababu ya ada na michango mingi mashuleni, kwa hiyo utekelezaji wa sera hii ulivyoanza, uandikishaji ukawa mkubwa, nafasi za wanafunzi kwenda sekondari zikawa nyingi kwa hiyo tukajikuta tuna upungufu wa vifaa kama hivi, lakini tunawashukuru ndugu zetu wa TASODA kwa mchango wao huu na tunawakaribisha wadau wengine kuendelea kuchangia sekta hii ili elimu ili iendelee kukua hapa nchini” Aliongeza Mwalimu Maganga.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Upendo Rweyemamu amewataka wanafunzi wa Sekondari hiyo kurudisha fadhira kwa wafadhili hao huku akiwaambia kuwa njia pekee ya kurudisha fadhira hizo ni kwa kusoma kwa bidi na kuongeza ufaulu katika mitihani yao.
“Matokeo mazuri ya mitihani yenu ndio shukrani pekee mnayoweza kuitoa kwa misaada hii, na mnajua kuwa mimi ni mtu wa kupiga kelele kuhusu matokeo, tulisha wekeana ahadi kuwa mwaka huu kidato cha nne hatutaona 'division zero', 'four' wala 'three', nataka tuone 'division two' pamoja na 'one' nyingi na ninaamini mnaweza” Alisisitiza Mwalimu Rweyemamu.
Aidha, Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Zedekia Agutu ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa jitihada za mara kwa mara za kuwapunguzia changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuwajengea madarasa.
Mwalimu Agutu Ameongeza kuwa shule yao ina jumla ya wanafunzi 1,046, kati yao wavulana ni 453 na wasichana ni 593, na kwamba baada ya msaada huo wa viti na meza 36 shule itabakia na uhaba wa meza 316 na viti 344.
Baadhi ya madawati na viti vilivyotolewa kusaidia kusaidia Shule ya Sekondari Mpunguzi.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpunguzi wakishangilia msaada wa madawati na viti walivyopewa na kikundi cha TASODA.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Josephat Maganga kushoto akimsikiliza Afisa Elimu ya Sekondari wa Jiji la Dodoma Upendo Rweyemamu wakati wa tukio la kukabidhiwa madawati na viti kwa Shule ya Sekondari Mpunguzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.