Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KIKUNDI cha vijana cha Taste tamu kimetakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa vikundi vingine katika kusimamia malengo ya kuanzishwa kwake na kuzalisha ajira katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jamal Ngalya alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutembelea na kukagua shughuli za kikundi cha vijana cha Taste tamu kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ngalya alisema kuwa amefurahia kukikuta kikundi kikiwa kinatekeleza majukumu yake. “Mimi natamani kuona vijana hawa wanakuwa ‘role model’ kwa vikundi vingine vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Tumeambiwa hapa mwenyekiti wa kikundi amesafiri kufuata mashine Dar es Salaam maana yake vijana hawa wanamaono makubwa katika kusimamia malengo yao” alisema Ngalya.
Naibu Meya alisema kuwa anafurahia kuona jinsi vijana hao walivyojiajiri na kuzalisha ajira nyingine kwa vijana wenzao. “Tumeona kikundi hiki kina vijana watano waliojiajiri. Jambo la kufurahisha vijana hawa wameajiri vijana wenzao watatu, maana yake wakikuza mtaji wataajiri vijana wengi zaidi na kutoa mchango wao kwa uchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na taifa kwa ujumla” alisema Ngalya.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kikundi cha Taste tamu, Katibu wa kikundi hicho, Wenseslaus Laurent alisema kuwa kiundi chake kimepata mafanikio baada ya kukopeshwa shilingi 20,000,000 fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Aliyataja mafanikio hayo kuwa ni kuagiza mashine za kuchakata matunda. “Mafanikio mengine tuliyoyapata ni kununua jokofu la kupoza juice na kuongeza pikipiki kwa ajili ya kusambaza bidhaa tunazotengeneza. Tumefanikiwa kuongeza wafanyakazi watatu kwa ajili ya kutafuta masoko. Vilevile, tumefanikiwa kununua mashine ya kuoka mikate” alisema Laurent.
Awali Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Viwandani, Farida Mayega alisema kuwa kikundi hicho kiliomba mkopo wa shilingi 40,000,000. “Mkopo waliopata ni shilingi 20,000,000 kwa kuwa ni mara yao ya kwanza. Ilikuwa ni lazima kupima uaminifu na uadilifu wao kwanza” alisema Mayega.
Kikundi cha vijana cha Taste tamu kinajihusisha na shughuli za ujasiliamali kilianzishwa mwana 2021 na kilikopeshwa shilingi 20,000,000 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji mwezi Juni, 2022 kwa lengo la kukuza mtaji wake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.