HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendeleza jitihada katika kukuza sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu na upanuzi wa shule Jijini hapa ikishirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) pamoja na taasisi nyingine za kifedha nchini.
TEA na Halmashauri ya Jiji la Dodoma zimrfanya hafla ya makabidhiano rasmi ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa shule za msingi Kisasa, Kizota, Medeli na Mlimwa C jana tarehe Mei 6, 2021 ambapo mradi huo unafanyika chini ya mshauri elekezi Chuo cha Sayansi Mbeya (MUST Consultancy Bereau - MCB) wenye gharama ya shilingi Bilioni 1.9 na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi minne kutoka sasa.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, iliyofanyika katika shule ya msingi Mlimwa C, Prof. Davis Mwamfupe amesema kuwa dhana ya Makao Makuu ina uwanda mpana na kuijenga inahitaji taasisi zote kushirikiana na kwamba suala la kutoa pesa ni jambo moja, kuzipokea na kuzielekeza katika matumizi sahihi ni jambo jingine la wa pili.
“Nakuagiza Mkurugenzi hatutegemei ucheleweshwaji wowote katika kutekeleza mradi huu, kucheleweshwa ni kuruhusu kukauka kwa zege, ucheleweshwaji ambao hauna maelezo hatutaukubali na kamati yangu ya fedha tunataka taarifa ya maendeleo ya mradi huu” alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEA Bahati Geuzye alisema kuwa, taasisi hiyo ya Serikali ambayo inafanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 8 ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia na kuratibu mfuko wa Elimu.
“Mamlaka inaanza rasmi utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya Elimu katika shule nne za msingi Jijini Dodoma kwa lengo la kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya Elimu, mradi huu ni miongoni mwa miradi 123 kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 ila ulichelewa kutokana na changamoto kadhaa lakini kwa sasa tumepata ufumbuzi na mradi unaenda kutekelezwa” alisema Geuzye.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa shule zitakafikiwa na mradi huo, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Medeli Grace Lisasi alieleza kiasi gani mradi huo ulivyo na faida kwani katika shule yake umefanya ufaulu kuongezeka toka asilimia 57 na kufikia asilimia 82 kutokana na mradi wa awamu ya kwanza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.