WASHIRIKI wa mafunzo ya Mpango wa Utayari wa Kumuandaa Mtoto Kwenda Shule (SRP) wametakiwa kuwahimiza Wasaidizi wa Walimu Jamii juu ya utengenezaji na utumiaji wa vitabu rahisi ili kupunguza gharama za ununuzi wa vitabu pamoja na kukidhi mahitaji ya vitabu kulingana na idadi ya watoto waliopo katika vituo vya utayari.
Kauli hiyo imebainishwa Jijini Dodoma na Mkuza Mtaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania Vida Ngowi ambae pia ni mwezeshaji katika mafunzo hayo.
Ngowi amesema Vitabu Rahisi ni vitabu vinavyotengezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali ambazo upatikanaji wake ni rahisi sana na matumizi ya vitabu hivyo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa vitabu katika vituo vya utayari.
"Tuendelee kuwahimiza Wasidizi wa Walimu Jamii jinsi ya kutengeneza na kutumia vitabu rahisi ambavyo vitawajengea watoto umahiri uliokusudiwa, na vitabu hivi sio mbadala wa vitabu vya kiada bali tunachukua yaliyomo katika vitabu vya kiada
Nasisitiza vitabu viwe imara,vitabu vitatengezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali zinazopatikana katika mazingira yetu mfano maboksi, manila na mengineyo" ameeleza Ngowi
Aidha, Ngowi amesisitiza juu ya ushirikishwaji wa watoto waliopo katika vituo vya utayari wakati wa kutengeneza vitabu rahisi, kwa ushirikishwaji utawajengea watoto tabia ya kupenda kutengeneza vitabu wao wenyewe pamoja na umahiri wa kusoma vitabu.
Naye Mwezeshaji na Mkufunzi kutoka katika Chuo cha Ualimu Nachingwea Mwl. Omary Patrick Sadick amewataka washiriki hao kuwahimiza Wasaidizi wa Walimu Jamii juu ya matumizi ya Shajara ya Taaluma ili kurahisisha utunzaji na upatikanaji wa kumbukumbu za ufundishaji na ujifunzaji katika Vituo vya Utayari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.