Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI imesema kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yatasaidia kuongeza uwezo wa utoaji elimu na kuongeza ufaulu kwa shule za sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA katika shule ya sekondari Chinangali iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo tarehe 16 Juni, 2022.
Waziri Nnauye alisema kuwa wizara yake kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) inakabidhi vifaa vya TEHAMA ili viweze kusaidia kuongeza uwezo wa utoaji elimu jijini hapa. “Ni matumaini yangu kuwa vifaa hivi vya TEHAMA vitaenda kuongeza uwezo wa utoaji elimu. Ufaulu utaongezeka, uelewa wa wanafunzi utaongezeka na uwezo wa kukabiliana na mazingira utaongezeka” amesema Waziri Nnauye.
Waziri huyo alitumia jukwaa hiyo kuiasa jamii juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya TEHAMA yasiyo sahihi. Alisema kuwa TEHAMA ina uwezo wa kusambaa na tamaduni za kigeni zikamharibu mtoto wa kiafrika kutokana na matumizi ya mtandao wa ‘Internet’.
Aidha, aliwataka wazazi kuwalinda watoto ili wasiharibiwe na maendeleo na kasi ya ukuaji wa TEHAMA. “Wazazi tusiwazuie watoto kutumia TEHAMA ila tuwalinde dhidi ya madhara yake. Tuwaambie watoto ukweli ili wawe huru” alisema waziri Nnauye.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde alisema kuwa siku hiyo ya mtoto wa Afrika ni ya kipekee. “Leo ni siku ya mtoto wa Afrika. Kipekee wananchi wa Dodoma tumepata heshima kubwa ya ugeni wako. Ni siku jamii inajikumbusha matukio yote yaliyompata mtoto. Tutahakikisha tunalinda na kusimamia watoto wetu ili wafikie malengo yao.
Aidha, alimshukuru Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuiwezesha shule hiyo kupata kompyuta. Alisema kuwa mpango wake ni kuziwezesha shule zote za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupata kompyuta.
Nae Afisa Elimu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alishukuru kuichagua shule hiyo kupata vifaa hivyo vya TEHAMA. “Ndugu mgeni rasmi, sisi tumefurahi sana. Tunashukuru sana kwa vifaa hivi, nikuhakikishie tutavitunza na mwakani vifaa hivi vitazaa matunda na kuongeza ufaulu” alisema Mwalimu Rweyemamu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.