Na. Dennis Gondwe, DODOMA
DIWANI wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede amesema kuwa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vilivyotolewa kwa Shule ya Sekondari Chinangali vitasaidia kutanua wigo wa matumzi ya TEHAMA shuleni hapo na kuwa chachu ya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
Kauli hiyo aliitoa wiki hii alipokuwa akitoa salamu za kata yake katika halfa fupi ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA katika Shule ya Sekondari ya Chinangali iliyofanyika shuleni hapo na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Naibu waziri wa Kilimo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde.
Diwani Ngede alisema “napenda kutoa shukrani kwa niaba ya wazazi na wananchi wa Kata ya Chamwino kwa mbunge wetu. Mheshimiwa mbunge uliahidi kuleta vifaa vya TEHAMA shuleni hapa na umetekeleza, shukrani kwa Mwenyezi Mungu akuwezeshe katika shughuli zako. Vifaa hivi kwetu ni vitendea kazi vitakavyotusaidia kutanua wigo wa matumizi ya TEHAMA shuleni hapa na kuchochea wanafunzi kupenda masomo ya sayansi”.
Kwa upande wa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alishukuru kwa Shule ya Sekondari Chinangali kuthaminiwa. “Ndugu mgeni rasmi nakushukuru sana kwa kututhamini na kuamua kufanya tukio hili Shule ya Sekondari Chinangali. Tunafahamu unazo shule nyingi nchini ila ukaamua kufanya hapa sekondari ya Chinangali” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Aidha, alisema kuwa anajivunia timu ya walimu wa shule hiyo wanaofanya kazi nzuri ya kufundisha na kuongeza ufaulu. “…shule hii ina wanafunzi 1,198 na walimu 45. Ninajivunia sana walimu hawa sababu wasipokuwepo sipo, natembea kifua mbele sababu yao” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alikabidhi kompyuta tano na projekta tano shuleni hapo na kuelezea faida na hasara za matumizi ya TEHAMA kwa wanafunzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.