MKURUGENZI wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Serikali imejipanga kuwa na mifumo miwili ya kujaza fomu ya uhiari wa kupata huduma ya chanjo ya Korona ikiwemo kupitia njia ya kielektroniki na njia ya karatasi.
Siku moja nyuma fomu ya kujaza kupata huduma ya kupata chanjo ilisambaa katika mitandao ya kijamii huku wananchi wengi wakihoji maswali mengi kuhusu utaratibu huo.
Hata hivyo Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichwale amesema fomu hiyo iliyotolewa katika mwongozo wa Serikali kuhusu chanjo ni ya kawaida na itakua inafafanuliwa vema kwa watakaohiari kupata chanjo na kuwasihi wananchi kupuuza taarifa za mitandaoni.
Dkt. Subi alizungumza leo Julai 15, 2021 ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya mlipuko wa tatu wa ugonjwa wa Korona na umuhimu wa chanjo ili kupambana dhidi ya ugonjwa huo.
“Utaratibu ambao Serikali imeuweka tutakuwa na mifumo ya aina mbili moja itakuwa ni mfumo ya kielektroniki ambapo mtu anaweza akatoa uhiari wake kwa kujaza mwenyewe kwamba anahitaji kwenda katika kituo fulani kupata chanjo za ugonjwa wa Covid-19,” alisema Dkt. Subi.
Aliendelea kusema kuwa, Wizara ya Afya, imekuwa ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma mbalimbali za tiba na kinga, hivyo kusisitiza kuwa baada ya utoaji wa elimu, mwananchi anakuwa na uhiari wa kupata huduma au kutopata.
“Tumekuwa tukiwapatia wananchi elimu ya kutosha juu ya huduma fulani, sasa ukishampatia elimu ya kutosha, mwananchi anakuwa na uhiari wa kupata huduma au kutoipata, sawasawa na mgonjwa anapoenda kufanyiwa huduma za upasuaji, tumekuwa tukimpatia huduma ya fomu ya uhiari,” amesema Dkt. Subi.
Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, hiari inaweza kuwa kwa njia ya mdomo au maandishi, hivyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona Serikali ikaona ni vizuri kwa Watanzania kuendelea kutoa hiari yao katika kupata huduma hizo za chanjo ya Korona.
Mbali na hayo Dkt. Subi aliwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa, chanjo za ugonjwa wa Korona ni bora, salama, zina ufanisi wa kutosha na zimeorodheshwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili ya matumizi ya dharura ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Korona.
“Chanjo hizi ni salama na zina ufanisi wa kutosha lakini pia ni bora, zimeorodheshwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili ya matumizi ya dharura hususan katika kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na wimbi kubwa la ugonjwa wa Covid – 19,” amesema Dkt. Subi
Amesisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kwa dhati kuutokomeza ugonjwa wa Korona na ndio maana inatumia afua zote za kupambana dhidi ya maambukizi ikiwemo uvaaji sahihi wa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi tiririka, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kutumia vipukusi, kufanya mazoezi na matumizi ya chanjo ya ugonjwa wa Korona.
Hata hivyo, Dkt. Subi amewatoa hofu Watanzania na kuwataka waendelee kuiamini Serikali na kufuata maelekezo yote kutoka kwa wataalamu wa afya katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, huku akisisitiza kuwa sayansi haiwezi kupindishwa na maneno ya mitandao ya kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.