WAWEZESHAJI ngazi ya Halmashauri watakaoshiriki zoezi la kuhakiki kaya masikini kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini wametakiwa kufanya kazi hiyo kwa weledi na kuhakikisha hakuna kaya hewa itakayosajiliwa.
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF na uhakiki wa kaya kwa wakuu wa idara na wawezeshaji ngazi ya Halmashauri yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya TASAF alisema “leo mnapokea mafunzo na kuwezeshwa, haya mkawaeleweshe wananchi kusudi zuri la serikali na nia njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu yao kwamba mkono wake haujawaacha unawagusa huko huko. Hatutaki kusikia kaya hewa katika ardhi ya Tanzania, halafu mtu (Afisa) akaendelea kukaa kwenye kiti kile alichopewa kukalia awawakilishe wengine huku amezungukwa na kaya hewa, hilo haliwezekani. Kitakachofuata hapa ni kutafuta maelezo ya kutosha kabisa ulifanyaje hii kazi, kama itaonekana na wewe ulikuwa sehemu ya kusababisha hilo liwepo, gharama yake ipo sambamba na miongozo, kanuni, taratibu na sheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hatutakubali, kwanza utazilipa hizo hela zote ulizosababisha ziende huko”. Amewataka kutenda kazi hiyo kwa haki na weledi kwa sababu ukifanya kazi njema Mungu humnyanyua mtu na kupata nafasi ya juu zaidi, aliongeza Dkt. Gwajima.
Katika kuhakikisha wawezeshaji ngazi ya Halmashauri wanatekeleza zoezi hilo la uhakiki kwa ufanisi, matumizi ya vishikwambi yatasaidia kubaini wale wote watakaohusika kukwamisha zoezi hilo. “Ndiyo maana kuna vishikwambi hapa ambavyo tutataka kujua kwamba nani alimuingiza huyu mtu kwamba ni kaya sahihi au si sahihi, maana watu wanafahamiana watalalamika. Sasa watakaposema, ufuatiliaji ukaanza itafahamika kwamba ni wewe au mimi nimefanya hiyo kazi tutakuwa tunazitia doa kazi zetu tulizopewa kwa niaba ya watanzania wengi waliopo nje ya ajira ambao hawana kazi ukapewa wewe hiyo kazi na hapo ndipo uchunguzi utakapoanza wa uadilifu wako ilikuwaje sasa mpaka ukakubaliana na hili. Huenda tukawa tumemuweka mtu ambaye si sahihi kutufanyia kazi za kuwakilisha watanzania milioni 60. Kwa hiyo iwapo hawa ma-WEO, na ma-VEO tutawatumia na kuwashirikisha vizuri tutafanikiwa” alisisitiza Dkt. Gwajima.
Aidha, aliwataka wakuu wa idara kusimamia vizuri utekelezaji wa zoezi hilo. “Lakini wakuu wa Idara hapa mmesimama nimewaona kwa nafasi zenu mkasimamie vizuri. Mimi sipati picha inakuwaje kwenye CMT mtu mkuu wa idara, wewe ni Afisa Mifugo unataka kutuambia habari za mifugo lakini hujui ni wana-TASAF wangapi ambao wanafuga na ng’ombe wao, mbuzi wao na kuku wao kama wapo hai hujui, lakini ni wewe ambaye unakwenda kufanya ‘supervision’ kule lakini hugusi hizi kaya, utarudije na ripoti yako nikaipokea, utatoa mrejesho gani kwa mkurugenzi? hiyo siyo sawa. Wewe ni mkuu wa idara ya Afya unakwenda kule kufanya shughuli zako za afya lakini suala la TASAF umeliweka pembeni halitoki kwenye taarifa zako hili ni tatizo. Kama wewe ni Afisa Kilimo halafu unakwenda kufanya shughuli za kilimo huna idadi ya wana TASAF kwenye maeneo yako wewe ni tatizo. Lakini wewe kama ni Afisa Ustawi wa Jamii unakwenda kufanya kazi za ustawi wa jamii lakini kwenye akili yako huna taarifa za watu wa TASAF ambao wanaendeleaje kwenye masuala ya ustawi wa jamii, wewe ni shida. Lakini wewe kama ni Mwanasheria na upo kwenye CMT umekaa watu wa TASAF wanadhulumiwa kule, wanalia hata hawajui waende wapi, kidogo walichopewa hawawezi kukifuatilia wenyewe lakini wameshadhulumiwa wewe nawe ni tatizo” alisema Dkt. Gwajima.
Mafanikio ya mpango wa TASAF yanategema ufahamu wa mfumo na kila mtu aweke agenda ya maendeleo, kuwa walengwa hao wakinyanyuka maendeleo yatapatikana. “Watu hawa wakinyanyuka wakafanya hata hatua mbili za maendeleo katika watu milioni saba, mara hatua mbili itakuwa ni milioni 14 watakuwa wametusogeza kama nchi na tutatoka kwenye uchumi wa kati na kwenda kwenye uchumi wa juu zaidi” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa katika mafunzo hayo wapo wawezeshaji 52 kutoka idara mbalimbali za Jiji la Dodoma. “Matumaini yangu ni kuwa mafunzo haya na zoezi hili litafanyika kwa uadilifu mkubwa na baada ya mafunzo haya matokeo chanya yataonekana. Hatutarajii kupata wanufaika hewa katika Jiji letu” alimalizia Kimaro.
Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF na uhakiki wa kaya kwa wakuu wa idara na wawezeshaji ngazi ya Halmashauri yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.