WATENDAJI Kata na Mitaa na watumishi wa Idara ya Mipango miji, Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili waweze kutoa huduma bora kutatua migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi katika kikao cha kazi baina yake na watendaji hao katika ukumbi wa J.K. Nyerere wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini - Dodoma.
Kunambi alisema kuwa jukumu la msingi kwa watendaji wote ni kuwahudumia wananchi kwa viwango stahiki. “Watendaji wa Kata na Mitaa timizeni majukumu yenu. Mkumbuke kuwa mna kofia mbili, ya Mkuu wa Wilaya na ya Mkurugenzi wa Jiji. Hivyo, lazima matatizo ya wananchi yawaguse na muone mnawajibu katika kuyatatua. Mkiona wananchi wengi wanakuja kwenye ofisi zenu mjue kuna matumaini wanayoyapata kutoka katika ofisi zenu. Ila mkiona hawaji na wanakimbilia kwa Mkurugenzi mjue hamtimizi wajibu wenu” alisema Kunambi.
Mkurugenzi aliwataka watendaji kufanya ukaguzi na kuzuia ujenzi holela katika maeneo yao. Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inajengwa katika karne ya 21 kwa kuzingatia taratibu za ujenzi na mipango miji. Kila ujenzi unatakiwa kufuata taratibu ikiwemo kupata kibali cha ujenzi ili kuepuka ujenzi holela. Aliwataka watendaji hao kuweka mpango wa kudhibiti ujenzi holela na kukagua uhalali wa vibali vya ujenzi katika maeneo yao yote.
Aidha, aliwataka watendaji kujiepusha na kuomba na kupokea rushwa katika utendaji wao wa kazi. Alisema kuwa sekta ya ardhi inalalamikiwa sana na wananchi na kuwa na migogoro mingi. “Migogoro mingi ya ardhi ni ya kurithi kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu. Na changamoto kubwa wananchi hawakuwa wakipata fursa ya kusikilizwa. Katika kutatua migogoro ya ardhi, Halmashauri ya Jiji imetoa viwanja mbadala na viwanja vya gharama nafuu zaidi ya 3,000 kwa wananchi. Hakuna eneo lolote nchini wananchi wamepewa viwanja bure, ni Dodoma pekee” alisema Kunambi.
Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wakati chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo kiliwakilishwa na Mkufunzi aliyetoa mada kuhusu Wajibu na Majukumu ya Watendaji wa Kata/Mitaa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walitoa mada kuhusu mbinu na mikakati ya kupambana dhidi ya rushwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.