Na. Coletha Charles, DODOMA
Timu ya Mpira wa Pete ya Elimu Msingi imeibuka na ushindi wa kishindo kwa kuifunga Timu ya Combine (Elimu Sekondari na Watendaji wa kata) kwa mabao 9-5 ambapo mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, ukiwa na ushindani mkubwa huku kila upande ukionesha mchezo wa hali ya juu.
Mchezo ulianza kwa kasi huku Timu ya Elimu Msingi ikiongoza katika robo ya kwanza kwa mabao 4-1 wakitumia uzoefu wa wachezaji wao wakongwe. Hata hivyo, Combine walionesha nidhamu ya hali ya juu na kutumia mbinu bora za kiufundi, katika robo ya pili timu zote ziliongeza kasi ili kupata alama muhimu za ushindi huo wa kihistoria.
Kocha wa timu ya Elimu Msingi, Emma Ernest, alisema kuwa, walishinda kwa sababu nyumba bila msingi hauwezi kujenga. Hivyo, waliweka msingi imara ndio maana waliweza kushinda kwa kishindo kwa kufanya mazoezi. “Tulijiandaa vya kutosha kwa mchezo huu. Wachezaji wangu wameonyesha nidhamu, umoja, na uwezo wa kupambana hadi dakika ya mwisho. Ushindi huu ni wa juhudi za pamoja. Tulijua kuwa mchezo utakuwa mgumu, lakini tuliweka mikakati ya kimpira na kisaikolojia ambayo iliwasaidia wachezaji wetu kuwa imara. Ushindi huu ni muhimu kwetu na tunajivunia mafanikio haya” alisema Ernest.
Kwa upande wake, Kocha wa Combine, Theopister Andrea, alikiri kuwa timu pinzani ilikuwa bora zaidi katika mchezo na timu yake ilikosa umakini katika upande wa wafungaji, lakini aliahidi atafanya marekebisho. “Tulijaribu kadri ya uwezo wetu, lakini Timu ya Elimu Msingi walikuwa na mpango mzuri wa mchezo. Tumepoteza nafasi muhimu ambazo zilitugharimu, lakini tutajitahidi kufanya mazoezi ya ziada ili tuwe bora zaidi katika michuano” alisema Andrea.
Nae, Nahodha wa Timu ya Elimu Msingi, Jane Thawe, alisema ushindi huo ulikuwa matokeo ya maandalizi mazuri na mshikamano wa timu na walijipanga kwa ajili ya mashindano haya. “Tulijitahidi sana, hasa katika robo ya mwisho. Ninamshukuru kila mchezaji kwa juhudi zake, Timu ya Combine wakati mwingine wajipange na sisi tunakikosi kipana kilichoingia leo ni kikosi ‘C’ tu na tulikuwa tunafanya mazoezi usiku na mchana kwa hiyo ushindi ni kawaida yetu” alisema Thawe.
Aidha, Nahodha wa Timu ya Combine, Evarista Mkalawa, alikubali matokeo kwa moyo wa sportsmanship na kuwapongeza wapinzani wao. “Walistahili kushinda, lakini tumejifunza mengi kutoka kwenye mchezo huu, tulizidiwa nguvu na wenzetu lakini tuko vizuri na katika mchezo ukifanya kosa moja mpinzani anatumia nafasi hiyo kukuadhibu, tumekubali tumeshindwa. Tunaahidi kurejea tukiwa imara zaidi” alisema Mkalawa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.