Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshauri kuundwa timu katika kila kata zitakayohusika kuvijengea uelewa vikundi vinavyokopeshwa viweze kurejesha mikopo kwa wakati ili wakopaji wengine waweze kunufaika.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu namba moja ya wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhe. Jaffar Mwanyemba alipoongea baada ya kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mhe. Mwanyemba alisema “tumeweza kufanikiwa kutembelea miradi sita ambayo ina uwiano tofauti. Tukichukulia vikundi vya watu wenye ulemavu na vijana waliokopeshwa ni kweli kwamba wamekopeshwa ila nadhani tunatakiwa tujiongeze. Huenda kwenye kata tuunde timu ambazo zitakuwa zinawapitia wanavikundi waliokopa, kuwakumbusha na kuwajengea ufahamu kuwa huo mkopo ni deni na wanatakiwa kurudisha ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wao kukopa tena au wengine pia waweze kukopa” alisema Mwanyemba.
Aidha, aliwataka waliokopa kulipa kwa mujibu wa mikataba ya mikopo waliyokopa. “Waliokopa waende sambamba na maandishi yaliyowawezesha kuweza kupata mikopo yao. Tujaribu kuwasumbua sana vinginevyo tutakuwa na mpango mzuri wa serikali kuwakopesha ila hautakuwa na maana kwa sababu hauna matokeo mazuri. Matokeo yake, fedha ya serikali itakuwa inapotea na serikali itakuwa haina fedha nyingine za kuwakopesha wanavikundi wengine wenye uhitaji” alisema Mwanyemba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Asha Vuai alisema kuwa wataalam wa wamepokea maelekezo na ushauri ya madiwani. “Leo tupo na ziara ya waheshimiwa madiwani wa Kamati ya Fedha na Utawala. Tumetembelea miradi mbalimbali ikiwemo vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Vikundi vinne vimetembelewa vya vijana viwili, kina mama kimoja na wenye ulemavu kimoja. Waheshimiwa madiwani wameshauri na wametoa maelekezo yao. Sisi kama wataalam tunaahidi tutayatekeleza kwa kuyafanyia kazi yale yote waliyoshauri” alisema Vuai.
Alisema kuwa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana inaendelea kuhamasisha vikundi ili viendelee kufanya marejesho kwa wakati. Vikundi vikifanya marejesho kwa wakati vinatoa fursa kwa vikundi vingine kuweza kukopeshwa, aliongeza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.