Na. Josephina Kayugwa, DODOMA
MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ametoa wito kwa watendaji wa kata pamoja na maafisa maendeleo jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwasaidia wananchi kwa kuwaelimisha juu ya mikopo inayotolewa na halmashauri bila kuchukua rushwa.
Wito huo ameutoa katika kikao kilichofanyika leo kwenye ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alipokutana na watendaji wa kata,watendaji wa mitaa na maafisa maendeleo ya jamii.
“Tunatakiwa tuamke kufanya kazi na tupambane kama viongozi, katika suala hili la mikopo kuna baadhi ya kata zimefanikiwa na nyingi bado nataka niwambie kuwa wale ambao bado mjifunze kwa wenzenu ambao wameshafikia hatua nzuri.
“Mko pale kwaajili ya kuwasaidia watu na hakuna mtu mwenye nguvu ya kuzuia vikundi kwaajili ya kupata mkopo kama kiongozi una vikundi vingi leta vyote na kikundi chenye sifa kitapitishwa ambacho hakina mnatakiwa kuwaelekeza nini cha kufanya ili na wao wapate mkopo,” alisema Mafuru.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Dodoma, Davis Mwamfupe alisema inatakiwa vigezo na masharti ya utoaji mikopo viangaliwe upya kwa kuwa kumekuwa na vikundi vikifanya udanganyifu kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi ili waweze kupata mkopo.
“Kuna baadhi ya watu hawatoi taarifa sahihi wakati wa kuomba mikopo na wengine wanakuwa hawana makazi maalumu ya kukaa wala kufanyia biashara kitu ambacho kinasababissha usumbufu wakati wa kufuatilia urejeshaji wa mikopo.
“Fedha nyingi zimekuwa zikipotelea mikononi mwa watu kwasababu kunakuwa hakuna taarifa sahihi na wengi wao wamekuwa wakikimbia na kwenda kusikojulikana kwahiyo kipengele cha taarifa za muombaji inabidi kiangaliwe kwa upya ili kuondokana na usumbufu,” alisema Mwamfupe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.