WANANCHI wa Dodoma watakiwa kulinda mazingira na kutoa taarifa kwa uongozi wa Kata, Mtaa au Ofisi za Halmashauri ya Jiji pindi wanaposhuhudia mtu au watu wakifanya uchafuzi wa mazingira wa aina yoyote ili taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi, Dickson Kimaro alipokua akiongea na waandishi wa habari.
Kimaro alisema kuwa swala la usafi ni ustaarabu na unatakiwa uanze na sisi wenyewe, kila mmoja awajibike kulinda mazingira kwa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka ni safi “kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara hasa wa maduka kufanya usafi kwenye maduka yao nakutupa uchafu kwenya mitaro ya maji ya mvua, pia wafanyabiashara wa chakula wamekua wakimwaga maji machafu kwenye mitaro hivyo, kusababisha mitaro kuziba hasa kipindi cha mvua. Dodoma tuna kampeni ya ‘Mita tano usafi wangu usafi wangu mita tano’ nitoe wito kwa wananchi ukiona mtu, mwenye duka, mwenye biashara au mwenye nyumba anafanya uchafuzi wa mazingira na kutupa taka hovyo kuzunguka eneo lako toa taarifa haraka kwenye Ofisi za Kata au Mtaa zilizopo karibu yako au tupigie simu ili tutume mgambo aende kumkamata kwaajili ya taratibu zingine za kisheria”.
Akiongelea hatua wanazozichukua kama jiji pindi wanapomkamata mharibifu wa mazingira alisema kuwa tunapofanya ukaguzi wa siku kwa siku kupitia maafisa Afya, Mazingira na Polisi Jamii waliopo kwenye kata, wamekuwa wanawachukulia hatua wakiwakamata waharifu kwa kuwatoza faini ya kuanzia shilingi 50,000/= hadi 300,000/= kutegemeana na ukubwa wa tatizo alilosababisha kwenye uharibifu wa mazingira.
“Ingawa kumekuwa na baadhi ya wananchi wamekuwa wakiharibu mazingira kwa kutupa takataka kwenye mitaro ya maji ya mvua , wengine wamekuwa wakikusanya takataka kwenye nyumba zao na kuchoma katikati ya mitaro licha ya jitihada tunazozifanya. Tumechukua hatua kubwa sana kwa mwaka wa fedha uliopita kwenye kipengele cha uchafuzi wa mazingira pekee tumekusanya zaidi ya milioni 46 kupitia faini mbalimbali za uchafuzi wa mazingira” alisema Kimaro.
Alimalizia kwa kuwashauri wakazi wa Dodoma kuwa na kasumba ya kupenda usafi na kushiriki kwenye shughuli za usafi wa mazingira sababu wamepata dhamana kubwa sana yakuidhinishwa kuwa jiji hivyo, wanatakiwa kuwa jiji la mfano kwa kuhakikisha mazingira yao ni safi na salama.
“Niwaombe wakazi wa Dodoma kuwaunga mkono viongozi wa kata na mitaa ambao wanawajibu wa kusimamia usafi kwa kujitokeza kwa wingi kila Jumamosi kushiriki zoezi la usafi wa mazingira katika mitaa yenu. Kwa pamoja tunaweza kuyatunza mazingira yetu na kuifanya Dodoma kuwa jiji safi” alimalizia Kimaro.
Kwa upande wake Elia Nyoni, mkazi wa mtaa wa Kizota aliupongeza uongozi wa Jiji la Dodoma kwa kuhakikisha maeneo ya umma na wazi kama makaburi yapo safi “kusafisha maeneo kama hayo ni ibada kwa sababu tunasafisha na kuweka safi maeneo ambayo wenzetu wamelala. Sasahivi ukienda makaburi ya Kizota ni masafi nawapongeza sana kwa kuyapa kipaumbele maeneo ya umma kwenye usafi. Niwaombe wanadodoma wenzangu tuendelee kuwaunga mkono katika shughuli za usafi na kutoa taarifa sehemu husika kwa wote wanaovunja sheria za mazingira” alisema Nyoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.