HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kuendelea kutoa habari za utekelezaji wa majukumu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufahamu muelekeo wa Halmashauri yao katika utoaji wa huduma bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akiongelea tukio la kihistoria la kufikisha idadi ya watu (viewers) wanaotembelea tovuti ya Jiji kufikia 500,000 ofisini kwake leo.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano kinawajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa habari na taarifa kwa wananchi likiwa ni takwa la Kikatiba Ibara ya 18 (b) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kisheria Ibara ya 5 ya Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya Mwaka 2016. “Kupitia takwa hilo, tovuti ya Halmashauri inatakiwa kutoa taswira halisi ya Halmashauri, utendaji, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wananchi. Hivyo, tovuti ya Halmashauri ni Halmashauri iliyorahisishwa kupitia Teknolojia ya Habari” alisema Fungo kwa msisitizo.
Fungo alisema kupitia umuhimu huo wa utoaji habari na taarifa “idadi ya watu wanaotembelea tovuti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma www.dodomacc.go.tz ilifikia 500,000 jana tarehe 22 Oktoba, 2020. Haya ni mafanikio makubwa kwa Halmashauri yetu. Aidha, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku. Leo tarehe 23 Oktoba, 2020 tunao watembeleaji 504,993. Hadi muda huu saa 11:15 watu ambao wametembelea tovuti yetu wamefika 2,626 na wanaoendelea kutembelea sasa hivi ‘online’ 63”.
Mafanikio haya ya kihistoria yanaonesha kuwa watu wanakiu ya habari na taarifa za halmashauri. “Idadi hii kubwa ya watu wanaotembelea tovuti yetu ni ishara kuwa wanaimani na habari na kazi nzuri inayofanywa na halmashauri yetu. Wajibu wetu ni kuendelea kutoa habari na taarifa mbalimbali zenye ubora katika tovuti ya Halmashauri ili kuwapa watembeleaji kile wanachostahili” alisema Fungo.
Aidha, Fungo ametoa shukurani kwa watembeleaji wote wa tovuti hiyo, menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na watumishi wa Jiji la Dodoma kwa michango yao na pia watumishi wote wa kitengo anachokiongoza. Amewasihi watembeleaji wa tovuti hiyo kuendelea kutembelea na akatoa nafasi ya wao kushauri mambo ambayo yatasaidia kuboresha maudhui ya tovuti hiyo. "Watu wanaweza kutuma maoni yao kirahisi kwa kubofya sehemu iliyoandikwa 'Wasiliana nasi' ambayo ipo juu ukifungua tovuti" alishauri Fungo.
Akiongelea tofauti ya tovuti ya Jiji na tovuti nyingine alisema kuwa ni habari zinazotolewa haraka kwa kuzingatia viwango vya uandishi wa habari na taarifa. “Ukiangalia wakati sisi tumepindukia watembeleaji tovuti 500,000, Halmashauri inayotufuata inawatembeleaji chini ya 100,000 kwa upande wa Halmashauri za Majiji” alisisitiza Mkuu huyo wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, QS Ludigija Ndatwa alisema kuwa tovuti ya Jiji kwake ni darasa. “Mimi ni mtembeleaji mzuri wa tovuti hiyo karibu kila siku naitembelea. Mara nyingi huwa nataka kujua taarifa mpya za matukio mbalimbali zilizoingia kwenye tovuti ya Jiji. Bahati nzuri huwa nazikuta” alisema QS Ndatwa.
Kutembelea tovuti hiyo kumemsaidia kujifunza na kufahamu mambo mengi yanayofanyika katika idara nyingine za Halmashauri ambazo isingekuwa rahisi kuzipata kwenye vikao. “Mfano utaratibu wa kupata kibali cha ujenzi, mtu akiniuliza huwa sihangaiki hata kumuelezea, namwambia tembelea tovuti ya Halmashauri utakuta utaratibu wote” alisema QS Ndatwa kwa kujiamini.
Ikumbukwe kuwa tovuti za Halmashauri zilizinduliwa tarehe 27 Machi, 2017 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.