Taasisi ya sekta binafsi Tanzania imeahidi kuunga mkono Juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma za kuvutia wawekezaji kuwekeza jijini hapo na kuzalisha ajira.
Ahadi hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta binafsi Tanzania, Zachy Mbenna (pichani), alipokuwa akiongea katika mkutano wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania "Private sector breakfast meeting" uliofanyika katika hoteli ya Dar es salaam Serena mwishoni mwa wiki.
Mbenna alisema “agenda ya kuvutia wawekezaji Halmashauri ya Jiji la Dodoma tutaiweka kwenye agenda zetu za kudumu kutokana na hii heshima kubwa ambayo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetupatia, tutakuwa mabalozi wazuri kwa kuvutia wawekezaji. Tunaamini kupitia nyie hakuna muwekezaji atakayeumizwa” alisema.
Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na halmashauri hiyo katika kufanikisha agenda hiyo, pamoja na kuialika halmashauri hiyo katika mikutano mbalimbali itakayokuwa ikiendeshwa na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fred Robert wakati akiwasilisha mada juu ya fursa za uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, alisema kuwa Halmashauri hiyo imekamilisha Mpango Kabambe (Master Plan) ulioainisha fursa za uwekezaji katika Jiji hilo kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii, uwekezaji na kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umeainisha maeneo ya uwekezaji katika nyanja za elimu, afya, biashara, kilimo, burudani pamoja na mengine” alisema Robert.
Akiongelea uwekezaji katika sekta mbalimbali, alizitaja kuwa ni elimu na kusema maeneo ya uwekezaji yapo katika ujenzi wa vyuo, shule na maeneo ya michezo. “Kwa upande wa Afya, maeneo yaliyopimwa yapo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Vilevile, yapo maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, hoteli na maduka makubwa yaani shopping malls” alisema Robert.
Maeneo mengine ya uwekezaji aliyoyaelezea ni kilimo cha kisasa katika maeneo ya Jiji (urban agriculture) na uwekezaji katika maeneo ya Ranchi.
Timu ya kimkakati ya kutafuta masoko ya miradi ya uwekezaji ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ipo katika ziara ya kutafuta wawekezaji Jijini Dar es Salaam kwa wiki nzima.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.