Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ambapo kwa mwezi Septemba imevuka lengo la makusanyo na kuvunja rekodi ya miaka 23 iliyopita.
Tangu ilipoanza kufanyakazi Julai Mosi 1996, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevunja rekodi kwa kukusanya Sh1.76 trilioni Septemba 2019.
Makusanyo haya ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.2 ya lengo la TRA kukusanya Sh1.81 trilioni iliyojiwekea mamlaka hiyo.
Yakilinganishwa na Septemba 2018, makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 29.18 hivyo kuzidi ufanisi wa miezi yote ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.
Kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Edwin Mhede amesema makusanyo haya ni kiashiria wananchi wameelewa, wamekubali na kuitikia wito wa Serikali kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Julai tulikusanya Sh1.25 trilioni sawa na asilimia 91.92 ya Sh1.36 trilioni na Agosti tukapata Sh1.33 trilioni sawa na asilimia 96 ya Sh1.4 trilioni,” alisema Dk Mhede.
Kamishna huyo amewashukuru walipakodi waliojitoa kutii sheria na Serikali kwa kuendelea kuiunga mkono mamlaka hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kukusanya na kuhasibu mapato ya umma.
“Pamoja na mafanikio haya, tunajua kuwa bado hatujafikia malengo yetu. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha uendelevu wa ufanisi huu mkubwa kwa miezi ijayo,” alisema.
Mhede ni kamishna wa tano kuteuliwa na Rais John Magufuli ndani ya miaka minne iliyopita. Akiwa na miezi minne sasa tangu akabidhiwe jukumu hilo, alisema sababu zilizochangia kupanda kwa makusanyo hayo na kuvunja rekodi ya miaka 23 ya uwapo wa TRA ni kuzibwa kwa mianya ya ukwepaji kodi, matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) na mifumo rafiki ya ukusanyaji kodi.
Baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani Novemba 5,2015 ufanisi wa TRA iliyokuwa inakusanya wastani wa Sh85 bilioni kwa mwezi uliongezeka na mapato hayo kufika Sh1.3 trilioni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.