HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania katika kutekeleza mpango wa urejeshaji Maisha kwa wananchi waliopitiwa na mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora ili kuwaneemesha wananchi hao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma baada ya kikao cha wataalam wa taasisi hizo mbili wakati wakati wa utambulisho wa mradi huo.
Nabalang’anya alisema “kwanza niwapongeze TRC kwa mradi huu, ni mradi muhimu sana, naweza kusema kuwa ulipaswa kuanza kabla ya utekelezaji wa fidia. Kwa sasa fidia imeshatolewa kwa wananchi na madhara yake yameshaonekana kwa wananchi kutumia fedha kinyume na matarajio ya mradi na serikali kwa ujumla”.
Alisema kuwa, kama mwananchi alikuwa anamiliki mali kama nyumba au ardhi na baadae mali hiyo ikatwaliwa na akalipwa fidia ili akafanye kile ambacho kilifanyika mwanzo maana yake badala ya kuendelea alirudi nyuma. Alisema kuwa bado nafasi ipo ya kuwaendeleza wananchi hao, “Hatujachelewa, tulipoanzia tuanze kwa vitendo. Kikubwa TRC wamezungumzia program ya mafunzo ambayo ni jambo la msingi sana, hasa mafunzo ya ujasiriamali. Hivyo, tunatakiwa kutambua mahitaji ya mafunzo yanayohitajika kwa jamii, kuwajengea uwezo na kuwafundisha kutasaidia kuwarejeshea maisha” alisema Nabalang’anya.
Mkuu huyo wa Idara aliongeza kuwa baada ya Dodoma kuwa makao makuu, imekuwa na fursa nyingi za kiuchumi. “Dodoma sasa ni makao makuu ya nchi, hivyo mradi wowote ambao utaanzishwa na kusimamiwa vizuri utainua kipato cha mlengwa. Jiji la Dodoma tunaahidi ushirikiano wa kutosha wakati wote katika kufanikisha mpango wa urejesho wa maisha kwa walengwa” alisisitiza Nabalang’anya.
Kwa upande wake msimamizi wa masuala ya kijamii kutoka TRC, Joyce Ponera alisema kuwa kufuatia changamoto zilizojitokeza baada ya kulipa fidia kwa wananchi waathirika wa mradi wa SGR ni matumizi mabaya ya fedha za fidia, TRC imekuja na mpango wa urejesho wa maisha kwa wananchi hao. “Tutawapa mafunzo ya matumizi bora ya fedha yatakayowawezesha kufanya vitu ambavyo vitawaletea maendeleo” alisema Ponera.
Mbali na mafunzo ya usimamizi wa fedha, mafunzo juu ya matayarisho ya ardhi, upataji wa ardhi na ujasiriamali, aliongeza. “Mafunzo haya tutafanya kwa waathirika wa mradi pekee. Aidha, taasisi tutazoshirikiana nazo ni TASAF, SIDO, VETA na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyo katika mnyororo huo”, alisema Ponera.
Shirika la Reli Tanzania lilifanya kikao kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhusu mpango wa urejeshaji maisha kwa wananchi waathirika wa mradi wa reli ya kisasa SGR.
Wataalam kutoka TRC na Jiji la Dodoma walipokutana kujadili utekelezaji wa mpango wa urejeshaji maisha kwa wananchi waliopitiwa na mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora.
Msimamizi wa masuala ya kijamii kutoka TRC, Joyce Ponera alipokuwa akiongea kwenye kikao na wataalam wa Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.