TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) ina matarajio makubwa na uwajibikaji na nidhamu kwa walimu waliopo katika Jiji la Dodoma katika utendaji kazi wao ili kutoa taswira halisi ya wao kuwa makao makuu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi msaidizi Ajira na maendeleo ya Walimu, kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu, Mectildis Kapinga alipokuwa akielezea matarajio ya Tume hiyo kwa walimu waliopo katika Jiji la Dodoma kuwa kioo kwa walimu wote nchini.
Kapinga alisema “ni matarajio ya Tume ya Utumishi wa Walimu kuwa, kwanza walimu wa Dodoma watakuwa walimu wa mfano kwa sababu wao pia ni sehemu ya kuwaambia hata walio nje ya Dodoma kuhusu Tume na huduma tunazozitoa na wanazozipata lakini pia kwa sababu wanapata kwa ukaribu zaidi dozi tunayoitoa kuhusiana na masuala ya walimu. Tunaamini walimu wa Dodoma watakuwa walimu wenye nidhamu, walimu wanaowajibika na walimu wa mfano kwa nchi nzima”.
Alitoa wito kwa walimu nchi nzima kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika utendaji kazi na kuwa walimu wenye maadili na nidhamu ili waweze kuigwa na kada nyingine. “Sisi kama Tume, tutaendelea kusimamia maadili ya mwalimu nchini kwa lengo la kurudisha hadhi ya mwalimu ili tuwe na utumishi wa walimu uliotukuka kwa maendeleo ya Taifa na uchumi wa viwanda” alisema Kapinga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.