TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) imetakiwa kuhakikisha inasimamia kwa karibu maadili na nidhamu ya walimu pamoja na kuhakikisha uwepo wa msawazo sawa wa walimu kwa shule za mijini na za vijijini ili kuharakisha maendeleo ya elimu nchini.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Musa Ally Musa kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) wakati wa kufunga kikao kazi cha Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka katika ofisi 139 za wilaya pamoja na Menejimenti ya Tume hiyo.
Kikao kazi hicho kilichofanyika kwa siku nne mjini Morogoro pamoja na mambo mengine kililenga kuwajengea uwezo Kaimu Katibu Wasaidizi hao juu ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu uliotolewa hivi karibuni na TSC kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa BOOST.
Akizungumzia kuhusu ukiukwaji wa Maadili ya Ualimu, Katibu tawala huyo amesema kuna baadhi ya walimu ambao wanajipamba kupita kiasi jambo ambalo linasababisha wanafunzi badala ya kuzingatia masomo Huishia kuangalia mapambo ya mwalimu kitu ambacho pamoja na kuwa kinarudisha nyuma maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi, kinaondoa hadhi na heshima ya walimu.
“Mkemee masuala ya nidhamu, ninyi ndio wasimamizi wa nidhamu katika shule zetu. Kuna vitendo vinafanyika shuleni ambavyo vinaondoa hadhi ya mwalimu. Unakuta mwalimu amejipamba kupitiliza, usoni, mdomoni, machoni amepaka vitu kupitiliza, wengine pua zimetobolewa zimewekwa urembo mwingi. Mapambo haya yanaweza kumfanya mwanafunzi badala ya kusikiliza masomo akawa anamuangalia mwalimu tu, huo nao ni utovu wa nidhamu,” Katibu Tawala huyo amesema.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ya nidhamu ni utoro wa walimu ambapo ameeleza kuwa bado kuna walimu wanaoondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila taarifa na wengine wanafika shuleni lakini wanakuwa watoro wa vipindi vyao vya kufundisha.
Amesema utoro wa walimu umesababisha wanafunzi kutomaliza masomo yao ya muhula jambo ambalo linamnyima mwanafunzi haki yake ya kufundishwa na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
Kiongozi huyo pia, ameitaka TSC kusaidia kuzuia vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa kwa wanafunzi ikiwemo uhusiano wa kimapenzi, ubakaji, ulawiti, unyanyasaji pamoja na kuadhibu wanafunzi kinyume na taratibu huku akifafanua kuwa vitendo hivyo vinafanywa na baadhi ya walimu na vingine vinafanywa na watu wengine wa mitaani.
“Vitendo vya uzalilishaji, ubakaji, ulawiti, adhabu zisizozingatia taratibu bado vinaendelea kuripotiwa dhidi ya wanafunzi. Inawezekana ubakaji unafanyika nje ya shule lakini bado wapo walimu ambao wanajihusisha na vitendo vya udhalilishaji wa wanafunzi. Na hapa sio kwamba walimu wa kiume tu ndio wanaowafanyia wanafunzi wa kike, lakini siku hizi wapo walimu wa kiume wanawafanyia wanafunzi wa kiume, pia wapo walimu wa kike wanawafanyia wanafunzi wa kiume.”
“Tukiweza kudhibiti vitendo hivyo, sekta yetu ya elimu itaendelea kukua na kufikia katika vile viwango tunavyovitaka. Kwa hivyo, Tume mna jukumu kubwa sana kuhakikisha mnaendelea kutoa elimu kuzuia haya yasitokee. Lakini pale inapohitajika chukueni hatua bila kuchelewa ili tuwanusuru watoto wetu,” alisema Katibu Tawala huyo.
Vilevile, ameishauri Tume hiyo, kuhakikisha inatekeleza jukumu lake la kuhakikisha msawazo sawa wa walimu kwa shule za mijini na vijijini kwa kuwa kuna wimbi kubwa la walimu wanaotaka kuhama kutoka shule za vijijini kwenda shule zilizopo mijini kitu ambacho kinasababisha kudorora kwa elimu katika Halmashauri zilizoko pembezoni.
“Katika Mkoa wangu wa Morogoro ninapata maombi mengi ya walimu wanaotaka kuhamia Morogoro Manispaa. Na mimi nimekataa kuruhusu walimu kuhamia Manispaa. Tume ninawasihi tekelezeni jukumu hili ipasavyo, tukiacha hali hii iendelee tutadhoofisha maeneo mengine na kusababisha elimu kudorora kwa kuwa hayatakuwa na walimu wa kutosha kuweza kuhudumia wanafunzi,” amesema.
Akitoa neno la kumkaribisha Katibu Tawala huyo, Katibu wa TSC, Mwl. Palina Nkwama amesema kikao kazi hicho kimefanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo washiriki ili kuwawezesha kwenda kutoa mafunzo kwa walimu ngazi ya shule kuhusu Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha Maadili na uwajibikaji kwa walimu.
“Mafunzo haya yamehudhuriwa na jumla ya washiriki 170 wakiwemo wajumbe wa Menejimenti ya TSC Makao Makuu (11), Watumishi wa Tume Makao Makuu (20) pamoja na Kaimu Makatibu Wasaidizi kutoka ofisi zote za Wilaya 139,” amesema Nkwama.
Aliongeza kuwa mada zilizowasilishwa katika kikao kazi hicho ili washiriki hao waweze kutoa elimu kwa walimu katika ngazi ya shule ni: Mwenendo na Tabia njema ya mwalimu, wajibu wa mwalimu kwa mwanafunzi, wajibu wa mwalimu kwa taaluma yake, wajibu wa mwalimu kwa mkuu wake wa shule, wajibu wa mwalimu kwa watumishi wenzake, wajibu wa mwalimu kwa mwajiri wake, wajibu wa mwalimu kwa jamii, wajibu wa mwalimu kwa Taifa pamoja na ushiriki wa mwalimu katika siasa.
Kwa mujibu wa Nkwama, washiriki hao walipewa maelezo kuhusu ukiukwaji wa Kanuni za Maadili na Utendaji katika Utumishi wa Walimu na adhabu zinazoweza kutolewa dhidi ya ukiukwaji huo.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa ufadhili wa banki ya Dunia kupitia mradi wa BOOST ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwa na Shule Salama.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.