Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu.
Mollel ametoa wito huo leo Februari 10, 2022 wakati akizungumza na wafanyabiashara na wananchi katika soko la Mavunde lililopo Kata ya Chang’ombe jijini Dodoma wakati wa zoezi la usafi wa mazingira.
Dkt. Mollel amesema kuwa uchafu wa mazingira katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara na makazi yanasababisha magonjwa ya mlipuko ambayo endapo mwananchi ataugua atalazimika kutafuta matibabu na hivyo kuharibu bajeti ya familia na uchumi wao.
“Mkifanya mazingira yenu kuwa mazuri gharama ya kusafisha mazingira yenu ni kidogo kuliko gharama mtakazotumia kwenda kujitibu magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira.
“Mojawapo ya vitu ambavyo vitatuongezea uhai ni kufanya usafi, uchafu unapunguza umri wa kuishi kwa sababu watu wengi wanakufa mapema kwa sababu wanaugua magongwa yatokanayo na uchafu hivyo ni muhimu sote tufanye usafi,” alitahadharisha.
Aidha, Naibu Waziri huyo alisema ipo haja kwa Sheria ndogo za Jiji la Dodoma kuwabana wananchi katika usafi wa mazingira pamoja na upandaji wa miti kama wanavyofanya kwenye kuezeka mabati ya rangi katika nyumba zao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alisema kuwa kampeni ya kupanda miti inakwenda sambamba na usafi wa mazingira nchi nzima.
Alisema zoezi la usafi lililofanyika leo ni mwendelezo wa shughuli zilizopangwa katika wiki ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 itakayozinduliwa Februari 12, 2022 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Pia Bi. Maganga amewapongeza na kuwashukuru wadau mbalimbali wa mazingira walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za mazingira zinazoendelea jijini Dodoma kuelekea uzinduzi huo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.