MKUU wa Wilaya ya Dodoma Alhaj. Jabir Shekimweri amewataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kuupokea kuushangilia na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru pindi utakapoingia ndani ya Wilaya ya Dodoma.
Wito huo ameutoa alipokutana na waandishi wa Habari ofisini kwake kwa lengo la kuwakaribisha wananchi kupitia vyombo vya habari kushiriki kuupokea Mwenge wa Uhuru 2024.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa Mwenge wa Uhuru 2024 utaingia ndani ya Wilaya ya Dodoma tarehe 03 Julai, 2024 ukitokea Wilaya ya Chemba utakimbizwa umbali wa km 45. 9 utatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi saba yenye thamani ya shilingi 7,096,668,714.32.
“Ningependa kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wanadodoma wote tujitokeze kwa wingi, kwa hamasa na bashasha kubwa kuupokea Mwenge wa Uhuru utakapokuwa kwenye ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Dodoma katika wilaya yetu. Mwenge wa Uhuru utapokelewa shule ya sekondari John Merlin ukitokea Wilaya ya Chemba na baada ya makabidhiano utaanza kutembelea kwenye miradi”.
Akiongelea miradi itakayopitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Alhaj Shekimweri alisema Mwenge wa Uhuru 2024 Wilaya ya Dodoma utaweka Jiwe la Msingi kwenye miradi mitatu mradi wa Kituo cha vyombo vya Habari cha Dodoma Media Group wenye gharama ya shilingi Bilioni 1,000,000,000.00, Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo wenye gharama ya shilingi Bilioni 3,094,983,663.32 na Mradi wa ujenzi wa barabara ya Judiciary kilomita 02 wenye gharama ya shilingi Bilioni 2,409,187,951.00.
“Mbio za Mwenge wa Uhuru zitatembelea Mradi wa Bagamoyo garden wa Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira wenye gharama ya shilingi Milioni 25,700,000.00, Mradi wa TEMBEKEZA ENTERPRISES wenye gharama ya shilingi Milioni 50,000,000.00, Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Upimaji Nkuhungu wenye gharama ya shilingi Milioni 50,000,000.00 na kuzindua Mradi wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza (Dodoma English Medium (wenye gharama ya shilingi Milioni 458,047,800.00” alimalizia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.