WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko akizungumza na kutoa muda wa miezi mitatu kwa Tume ya Madini kufanya uchambuzi wa kina kwa waliohodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi, baada ya kipindi hicho yafutwe na kupatiwa wawekezaji wenye uhitaji. Ameyasema hayo katika ziara yake aliyoifanya mkoani Ruvuma.
Kufuatia mahitaji makubwa ya Makaa ya Mawe kwa ajili ya kuzalisha nishati duniani na kutokana na madini hayo hivi sasa kuwa moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali, Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ametoa muda wa miezi mitatu kwa Tume ya Madini kufanya uchambuzi wa kina kwa waliohodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi, baada ya kipindi hicho yafutwe na kupatiwa wawekezaji wenye uhitaji.
‘’Kuanzia leo wawe wameyaendeleza hata kwa kuingia ubia wa kuchimba na kampuni zenye uwezo, mitaji, vifaa na teknolojia kama wanaona hawana uwezo wa kuyafanyia kazi maeneo yao. Naielekeza Tume ya Madini baada ya muda huu kupita, wafute leseni hizo kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123‘’ Msipochukua hatua ninyi, mimi nitachukua hatua, lazima mkutano huu uwe wa kazi na matokeo,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.
Kauli ya Biteko imefuatia hoja iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas aliyesema kuwa zipo baadhi ya kampuni na watu binafsi waliohodhi maeneo yao bila kuyaendeleza na hivyo kuiomba wizara kuangalia suala hilo.
Itakumbukwa kuwa, hivi sasa dunia ina kipindi kifupi cha kutumia makaa ya mawe kama chanzo cha nishati kabla ya kuhamia kwenye teknolojia ya kijani (green technology). Aidha, Mkutano wa 27 wa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi unaendelea nchini Misri Tanzania ikiwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo.
Biteko ameyasema hayo Novemba, 15, 2022, mkoani Ruvuma katika Mkutano wa wadau wa madini ya makaa ya mawe ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaofanyika kila mwaka. Katika Mkutano huo, wizara iliazimia kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa madini kwa lengo la kujadili changamoto zinazoyakabili makundi mbalimbali ya wadau ili kuzipatia majawabu.
Vilevile, kutokana na Tanzania kuwa na rasilimali hiyo ya kutosha na kufuatia kuwepo kwa ukomo wa matumizi ya madini hayo ulimwenguni, Biteko amesisitiza kwamba, lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa rasilimali hiyo pamoja na kukuza ajira zinazotokana na sekta ya Madini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.