Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma umeipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa utekelezaji wa takwa la kisheria la kutenga asilimia nne kwa ajili ya mikopo ya vijana kutoka katika mapato ya ndani.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 14 Machi, 2020 na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma, Billy Chidabwa baada ya kupokea taarifa fupi ya hali ya ukopeshaji mikopo asilimia nne kwa vijana katika ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Chidabwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa amesema kuwa taarifa iliyowasilishwa ni nzuri inayoonesha dhamira njema ya Halmashauri kwa vijana. “Taarifa tumeona ni nzuri, tumeona mambo mazuri. Fedha zinatolewa kwa vijana kwa wakati na kwa uwiano wa kuridhisha. Pongezi kwa Halmashauri na Mkurugenzi. Tunamfahamu sana anafanya kazi nzuri” amesema Chidabwa.
Aidha, aliwataka vijana wanaonufaika na mikopo hiyo kufanya marejesho kwa wakati. “Hizi pesa ni ‘revolving fund’, ukirejesha unampa fursa na mwingine kukopeshwa na kunufaika nazo. Jukumu letu sisi ni kuwa mawakili wa changamoto katika jamii, amesema Chidabwa.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya mikopo ya asilimia nne kwa vijana kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya amesema kuwa Halmashauri imeendelea kuongeza wigo wa ukopeshaji vijana. Baada ya kuanza kutekeleza sheria ya kukopesha makundi matatu ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ilikopesha shilingi 2,859,230,000 kati ya fedha hizo shilingi 972,000,000 zilikopeshwa kwa vikundi vya vijana. Idadi ya vikundi vilivyokopeshwa amevitaja kuwa ni 174. “Mwaka wa fedha 2019/2020 tumekopesha awamu moja shilingi 853,000,000. Kati ya fedha hizo shilingi 357,000,000 vilikopeshwa vikundi 40 vya vijana” amesema Nabalang’anya.
Akiongelea changamoto katika ukopeshaji huo, amesema kuwa awali vikundi vya vijana vilivyokuwa vikiwasilisha maombi ya mikopo vilikuwa vichache. Baada ya kutoa elimu na hamasa kwa jamii, sasa muitikio ni mkubwa na idadi ya maombi ni kubwa kuliko uwezo ameongeza afisa huyo.
Kwa upande wake Katibu wa Hamasa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Wilfred Mgomela amesema kuwa ziara hiyo ni ya kimkakati ina lenga kukagua utekelezaji wa asilimia nne ya mikopo ya vijana kama inawafikia vijana. “Katika ziara hii tunakagua vikundi mbalimbali pamoja na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi”.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya (aliyesimama) akitoa taarifa fupi ya hali ya ukopeshaji mikopo asilimia nne kwa vijana jijini Dodoma kwa wajumbe wa UVCCM Mkoa wa Dodoma katika ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.