Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kulinda viwanda na pia kuwalinda walaji, kufuatia kuzindua bwawa lenye lita za ujazo wa bilioni 25 za maji tarehe 3 Agosti 2024 katika Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, kilichopo Mvomero, mkoani Morogoro.
Mhe. Rais amepongeza uwekezaji huo mkubwa wa ndani uliogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 155 na ambao umeendana na uhalisia wa mabadiliko ya tabianchi. “Mradi huu ni mahiri na makini, hivyo niwapongeze sana kwa kudhamiria kuongeza tena ujenzi wa mabwawa mengine mawili ambayo yataongeza ajira kwa vijana wetu,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Ziara hiyo ya Mhe. Rais katika Mkoa wa Morogoro imehusisha pia uzinduzi wa awamu ya tatu ya upanuzi wa mashamba ya sukari na umwagiliaji ili kuwa na kilimo cha uzalishaji wa kisasa. Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia amelakiwa na maelfu ya wananchi katika Wilaya ya Mvomero wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
“Tunalenga kufikisha sukari tunayozalisha Jamhuri ya Watu wa Kongo na nchi nyingine kwa kuzidi kuboresha miundombino ya usafiri na uzalishaji ili kupanua wigo wa masoko ndani na nje ya nchi kwa kuongeza tija,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Kiwanda hicho cha Sukari kimefunga mitambo ya kisasa 47 inayofanya kazi kati ya 112 inayopaswa kujengwa ambayo itaongeza uchakataji wa miwa kutoka tani 100 hadi 180 kwa saa; ambapo matarajio hadi kufikisha mwaka 2027 ni kuchakata tani 230 ya miwa kwa saa. Kiwanda hicho kimeomba Serikali isaidie upatikanaji zaidi ya umeme wa uhakika na ujenzi wa barabara ya lami.
Aidha, imeelezwa kuwa kiwanda hicho katika kuboresha mnyororo wa shughuli za kilimo cha uzalishaji wa miwa matarajio yake kwa mwaka 2027 ni kutoa ajira zaidi ya elfu 10.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.