Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha vyanzo vya mapato vya kodi ya majengo na kodi ya ardhi kwa lengo la kuziongezea uwezo kwa kukusanya mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Shukrani hizo zilitolewa na Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira alipokuwa akichangia rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 20204/2025 kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea vyanzo vipya vya mapato. ‘Property tax’ ni chanzo chetu tulichokuwa tunakiamini sana wakati bado tukiwa Manispaa. Chanzo hiki kilichukuliwa na serikali kuu lakini sasa Mheshimiwa Rais katurudishia. Chanzo hiki kitatuletea zaidi ya shilingi bilioni nne. Hivyo, ni hatua nzuri ya kuimarisha bajeti yetu Jiji la Dodoma. Chanzo kingine ni kodi ya Ardhi ambayo asilimia 30 ya mapato itarudi katika halmashauri. Vyanzo vyote hivyo ulivijumlisha vinakupa zaidi ya shilingi bilioni 8.8. Hivyo, ni ongezeko kubwa la bajeti” alisema Fundikira.
Aidha, alimshukuru Mstahiki Meya kwa namna anavyoendesha vikao vya Baraza la Madiwani. “Tunakushukuru na kukupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya katika Jiji la Dodoma. Tunawashukuru wataalam wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji kwa kazi kubwa waliyoifanya kutushauri sisi madiwani katika kwenda kwenye mtiririko unaofaa kwa kufuata sheria na kanuni katika kusimamia na kuendeleza shughuli za halmashauri. Niendelee kuwashukuru kutuandalia bajeti nzuri kupitia vikao vyetu mbalimbali madiwani wameshauri maeneo kadhaa na kuelekeza fedha ziende kwenye miradi ya maendeleo hasa inayowagusa wananchi moja kwa moja na kuhakikisha kero katika kata zinatatuliwa katika mwaka wa fedha 2024/2025” alisema Fundikira.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.