Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Dodoma Jiji FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ameeleza nia yake ya kuchukua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza nchini baada ya kufanikiwa kupanda ligi kuu kwa kuongoza kwenye kundi B la michuano hiyo.
Kocha Mbwana Makata ameyasema hayo leo kwenye mahojiano mbele ya waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya mchezo wa kutafuta Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) utakaochezwa kesho saa 10 jioni kwenye dimba la Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam dhidi ya washindi wa Kundi A timu ya Gwambina FC ya jijini Mwanza.
Makata, kocha ambaye amejitengenezea wasifu mkubwa katika soka la Tanzania katika miaka ya karibuni, amefanikiwa kuziongoza timu tatu tofauti kwa misimu mitatu mfululizo kutoka ligi Daraja la Kwanza na kufanikiwa kuzipandisha kuingia Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akiuelezea mchezo wa kesho, Makata amesema wanataraji mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa Gwambina ni timu nzuri na imefanya vizuri katika kundi lao, "Tunawaheshimu Gwambina, wana timu nzuri, lakini tuna timu nzuri ya ushindani na tumekuja kuwaonesha kuwa sisi ni wazuri zaidi," amesema Makata.
Naye nahodha wa timu ya Dodoma Jiji FC Mbwana Kibacha amesema "wachezaji wote wako tayari kwa mpambano wa kesho, na wana morari ya juu kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kubeba ubingwa na kuwapa mashabiki wao furaha". Kibacha ameongeza kuwa wamejiandaa vya kutosha na wanataka kudhihirisha uwezo wao kwa kucheza soka safi na la ushindani.
"Tulifika salama na tumefanya mazoezi ya kutosha kujiweka sawa na mchezo huo, benchi la ufundi chini ya kocha mkuu wamefanya kazi yao, na sisi tuna deni la kutekeleza kile ambacho tumefundishwa ili kupata ushindi" aliongeza Kibacha.
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuelekea mchezo wao wa fainali ya ligi daraja la kwanza dhidi ya Gwambina FC.
Nahodha wa timu ya Dodoma Jiji FC Mbwana Kibacha akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya maandalizi na mikakati yao kwa mchezo wao wa kesho dhidi ya Gwambina FC ya jijini Mwanza.
Taarifa zilizotufikia katika meza yetu ya habari zinaeleza kuwa tayari viongozi na wapenzi wa Dodoma Jiji FC wameshaanza kuwasili jijini Dar es Salaam kutokea Jijini Dodoma na wengine wataingia kesho ili kuipa hamasa na kuishangilia timu yao.
Kila la heri Dodoma Jiji FC katika mchezo wa fainali ya ligi daraja la kwanza ngazi ya taifa hapa nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.