Na Josephina Kayugwa, DODOMA.
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kufuata sheria za kunawa mikono ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama vile Kipindupindu, Mfumo wa hewa na Macho. Sheria hizo ni kama vile kutumia maji safi na salama yanayotiririka, sabuni, kusugua mikono kwa sekunde 15 pamoja kujifuta kwa kutumia kitambaa safi
Ametoa wito huo katika maadhimisho ya Siku ya kunawa Mikono duniani ambapo katika wilaya ya Dodoma yamefanyika leo tarehe 15 Oktoba, 2022 katika Kata ya Mtumba yakiongozwa na kauli mbiu inayosena “Tuungane pamoja kuhakikisha usafi wa mikono kwa wote.”
Alisema katika kuzuia magonjwa ya mlipuko kila mtu anatakiwa kunawa mikono bila kusahau kufuata utaratibu na sheria zote ambazo zinahitajika kwasababu wengi wamekuwa hawafuati, hivyo hata wakinawa bado vimelea vya magonjwa vinakuwepo katika mikono yao.
“kila mtu anatakiwa kumlinda mwenzake dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwasababu gonjwa likimpata mmoja basi kila mtu itamuathiri maana magonjwa haya ya mlipuko huambukiza mtu mmoja baada ya mwingine na husambaa kwa haraka.
Lakini pia katika vituo vya afya pamoja na sehemu ambazo zinafanya watu wakusanyike basi sehemu hizo Maafisa afya wahakikishe vifaa vya kunawia mikono vinakuwepo muda wote ili viwasaidie watu kutekeleza jambo hili na naamini tutakuwa salama sote,” alisema Shekimweri.
Kwa upande wake Jacobo Ezekieli, Mkazi wa kata ya Mtumba alisema wananchi wafanye zoezi hili kwa amani kwa kushirikiana na viongozi wote wa kata bila kusahau kuelimisha ili kila mtu awe na elimu juu ya kunawa mikono.
“Sisi kama wananchi tunatakiwa kuwa pamoja na viongozi wetu ili tufanikishe jambo hili kwasababu magonjwa ya mlipuko ni hatari kwa afya zetu lakini pia kila mmoja wetu ana wajibu wa kumwambia ukweli mwenzake ili tulindane kama jamii dhidi ya magonjwa hatarishi,” alisema Ezekiel.
Aidha, aliwaomba viongozi wa Dini kuendelea kuwahamasisha waumini wakiwa katika sehemu zao za ibada kuzingatia jambo la kunawa mikono kwa kufuata sheria hata wakiwa majumbani kwao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.