Na Getruda Shomi, DODOMA.
MKUU wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro ametoa wito kwa wananchi wa Jiji hilo kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza lakini pia wajiepushe na ukataji miti ovyo ili kuunga mkono kampeni ya mazingira ya kukijanisha Dodoma.
Wito huo aliutoa ofisini kwake alipokuwa akifanya mahojiano maalum kuhusu zoezi la upandaji miti katika Shule ya Wasichana ya Bunge iliyopo Kata ya Kikombo jijini Dodoma.
Kimaro alisema wananchi wa Dodoma wapande miti kwenye maeneo yao ya makazi na sehemu za ujenzi kwa sababu miti hiyo itakuwa na manufaa kwao. “Nipende kutoa wito kwa wananchi wa Dodoma kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe anapanda miti isiyopungua mitano, mitatu ya matunda na mingine miti ya kivuli ili kuwapa faida za chakula na kivuli” alisema Kimaro.
Zoezi la upandaji miti limeandaliwa na Taasisi ya Kidini ya Shia Ismailia kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuunga mkono kampeni ya Kukijanisha Dodoma
Zoezi hilo la upandaji miti litafanyika Septemba 26, 2021 siku ya jumapili ambapo inategemewa kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mtendaji wa Kata, Taasisi ya Shia Ismailia, Mkuu wa Shule, walimu na wanafunzi wa Shule ya wasichana ya Bunge na wananchi wa Kata ya Kikombo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.