Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt. Hassan Abbas amesema, Serikali imetumia zaidi ya sh. bilioni 336/- kutekeleza miradi ya maji na upatikanaji wa maji umeongezeka sana.
Amesema jijini Dar es Salaam kuwa, upatikanaji maji vijijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 46 hadi 65% hivi sasa.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas hadi Septemba mwaka huu Serikali ilikuwa imekamilisha zaidi ya miradi 289 ya maji.
“Kwenye hiyo miradi kuna vituo zaidi ya elfu 89 kwa sababu unaweza ukajenga mradi ni tanki na chanzo cha maji lakini mradi mmoja ukawa na vituo zaidi ya mia mbili ambapo wananchi wanapata maji” amesema wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, miradi mikubwa 17 ya maji imekamilika mijini iliyogharimu zaidi ya sh bilioni 823/- na miradi ya maji zaidi ya 35 inaendelea kutekelezwa na kwa wastani upatikanaji maji mijini hivi sasa ni wastani wa 80%.
“Tupo vizuri, tupo pazuri lakini bado sisi tunawahimiza watendaji wetu na kwa niaba ya Watanzania kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa kasi, nidhamu na uaminifu ili asilimia 95 hata ikiwezekana kufikia mwaka 2020 tuweze kufikia hata 100% kwenye miji kwa hiyo ni kazi inayoendelea” amesisitiza Dkt. Abbas.
Dkt. Abbas amekumbusha kuwa, mwaka 2015 Serikali iliweka lengo la kufikisha maji 85% vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2020.
“Kazi kubwa inaendelea na mtakuwa mmeona mageuzi ya kitaasisi yaliyofanyika serikalini kwa mfano sasa hivi wale 'mainjinia' wataalamu wa maji wanawajibika moja kwa moja kwenye Wizara ya Maji hii yote ni kuongeza ufanisi na usimamizi unakuwa wa karibu” amesema Msemaji Mkuu wa Serikali.
Dkt. Abbas amesema, vituo 44,000 vya maji vinaendelea kujengwa na kwa wastani upatikanaji wa maji umeongezeka sana.
Chanzo: habarileo.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.