WANANCHI wa Wilaya ya Dodoma wametakiwa kuitikia rai ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ili wawe sehemu ya kurahisisha mchakato wa maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi na wafanyabiashara wa Kata ya Majengo waliojitokeza kwa wingi baada ya kushiriki zoezi la usafi wa mazingira.
Shekimweri alisema “ninawapongeza nyote kwa kujitokeza kwa wingi kufanya usafi. Leo ni tarehe 23 mwezi Julai, siku 30 kamili itakuwa tarehe 23 Agosti, ni siku ya Sensa ya Watu na Makazi. Nataka kuwaomba kuitikia rai aliyoitoa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwamba kila mmoja ahamasike na kuhamasisha mwingine kuhesabiwa. Tuweze kufahamu Tanzania kuna watu wangapi, wana hali gani za maisha na tena kwa mara ya kwanza mama huyu shupavu anafanya tu siyo Sensa ya Watu lakini pia anahesabu makazi”.
Alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lifanyike kwa ufanisi na haraka kwa kujaza madodoso kupitia vishikwambi.
Akiongelea umuhimu wa zoezi hilo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa litasaidia kuleta maendeleo. “Sensa hii itasaidia kwenye kutafsiri mahitaji ya kisera na mipango ya maendeleo na mgawanyo wa fedha za serikali kwa kuakisi hali halisi ya mahitaji ya wananchi” alisema Shekimweri.
Akiongelea utofauti wa Wilaya ya Dodoma na maeneo mengine, alisema kuwa imenufaika sana na bajeti ya serikali. “Sisi wana Dodoma tuna kila sababu ya kujitokeza kwa wingi zaidi kwa kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi makubwa ya kupaisha mkoa wetu na wilaya yetu. Sisi ni wanufaika wakubwa sana wa bajeti ya kiserikali. Lakini bado yapo maeneo yenye changamoto, inawezekana takwimu za huku nyuma hazikuwa na uhalisia wa watu walivyo, tujitokeze ili baadae tusilaumu mbona sisi tuna watu wengi lakini hakuna zahanati, tuna watu wengi lakini shule hazitoshi. Inawezekana kuna watu wengi, lakini kwenye Sensa hawakujitokeza kwa hiyo takwimu zilizopo ni za watu wachache” alisisitiza Shekimweri.
Shekimweri ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya Watu na Makazi Wilaya ya Dodoma aliyataka makundi yote kushiriki kikamilifu. ”Ni muhimu sana makundi yote kwenye kaya zetu na familia zetu kujitokeza kuhesabiwa. Tusinyanyapae na kuwaficha watu wenye ulemavu. Kuna haja ya kufahamu wenzetu wenye ulemavu ni wangapi ili mipango ya serikali iweze kuwafikia” alisisitiza Shekimweri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.