Kikundi cha Vijana TUSUMUKE kinajivunia mashine bora za kutotolesha vifaranga vya kuku zikiwa na uwezo wa kutotolesha vifaranga zaidi ya 30,000 kwa mwezi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa kikundi hicho, Erick Tigelindwa alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kikundi kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyotembelea kikundi hicho jana kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Tigelindwa alisema “kikundi kina mashine bora za kutotoresha vifaranga vya kuku zenye uwezo wa kuzalisha vifaranga 31,000 kila mwezi”. Katika kuhakikisha kikundi kinawahudumia vizuri wateja wake, kimefanikiwa kununua mashine ya kisasa ya kusaga nafaka kwa ajili ya kutengenza chakula cha kuku na samaki.
“Kikundi pia kina mashine ya kuchanganyia chakula cha kuku yenye uwezo wa kuchanganya tani moja kwa wakati mmoja” aliongeza Tigelindwa.
TUSUMUKE waliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kukiwezesha mkopo usio na riba kiasi cha shilingi 30,000,000.
“Mheshimiwa Mwenyekiti wa kamati na wajumbe wa kamati, kwa namna yoyote ile kikundi chetu cha TUSUMUKE hakiwezi kusema mafanikio yetu bila kukiri uwezeshwaji wa fedha ambazo ni mkopo kiasi cha shilingi 30,000,000 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma chini ya Mkurugenzi na watendaji wake. Fedha hii imekuwa chachu ya kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya kikundi chetu” alisema Katibu wa kikundi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Vedasto Ngombale aliushauri uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwatafutia vijana hao eneo la kurasimisha shughuli zao. Alipongeza kwa mawazo yao ya kuanzisha na kutekeleza miradi katika kikundi hicho. Aidha, alimtaka mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali kukagua hesabu za kikundi hicho kwa mujibu wa sheria.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa Halmashauri yake imepanga kukopesha shilingi bilioni 3.3 katika mwaka wa fedha 2019/2020. “Hadi kufikia sasa Halmashauri imekopesha shilingi milioni 855 mwaka huu” alisema Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.