Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WADAU wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 jijini Dodoma wameshauriwa kutoa elimu fasaha ya kujikinga na ugonjwa huo ili kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya ya Dodoma mjini, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na wajumbe wa kamati hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo.
Shekimweri amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na mapambano ya wimbi la tatu la ugonjwa wa UVIKO-19. “Sisi Wilaya ya Dodoma, tunahitaji kupeana elimu sahihi ya kinga ya UVIKO-19 kwa kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka safi na sabuni. Tunatakiwa kuwaambia wananchi ukweli kuwa aina na jinsi ya kuvaa barakoa na inatakiwa ivaliwaje na kwa muda gani” alisisitiza Shekimweri.
Shekimweri ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini alisema kuwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 yanaongozwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. “Mapambano haya sio ya mtu mmoja, bali ni yetu sote. Tunataka baada ya kikao hiki tutoke na mkakati jumuishi wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika wilaya ya Dodoma mjini” amesema Shekimweri.
Akiwasilisha taarifa ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method amesema kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Korona. “Virusi hivi vya Korona ni virusi vipya, tofauti na virusi vingine vya jamii hiyo vilivyowahi kusababisha mlipuko wa magonjwa kama ‘SARS-CoV’ mwaka 2003 na MERS-CoV corona mwaka 2013” amesema Dkt. Method.
Akiongelea wimbi la tatu la maambukizi ya UVIKO-19, Mganga Mkuu huyo amesema kuwa halmashauri imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na wimbi la tatu la UVIKO-19. Akiyataja mapambano hayo, ameyataja kuwa ni kupokea na kusimamia miongozo mbalimbali inayoelekeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo. “Kusimamia uvaaji wa barakoa kwa watu wote na kusimamia utumiaji wa vitakasa mikono. Nyingine ni kusimamia unawaji wa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni” amesema Dkt. Method.
Halmashauri imekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kwa kutumia redio na kuelimisha jamii katika taasisi mbalimbali pamoja na vikundi vya bodaboda, nyumba za ibada, masoko, stendi za mabasi na daladala” ameongeza Mganga Mkuu.
Halmashauri imeshiriki kusambaza na kubandika mabango sehemu mbalimbali zenye jumbe za kujikinga na UVIKO-19. “Taasisi mbalimbali kama shule zimepewa elimu ya afya kuhusiana na UVIKO-19 na kusisitizwa kufuata mwongozo uliotolewa na wizara ya afya wa kujikinga na ugonjwa huo” ameongeza Dkt. Method.
Wilaya ya Dodoma mjini ilipata maambukizi ya UVIKO-19 wimbi la kwanza mwezi Machi mpaka Julai, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.