Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKOA wa Dodoma ulipata madarasa 776 pamoja na samani zake ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu ya elimu mkoani hapa.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga alipokuwa akitoa neno kuhusu tuzo za taaluma Mkoa wa Dodoma katika hafla ya utoaji tuzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha Nne mwaka 2021 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF jijini Dodoma.
Dkt. Mganga alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta ya elimu nchini. “Serikali inatekeleza mpango wa elimu ya msingi bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha Nne. Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kiwango kikubwa. Kupitia fedha za mapambano dhidi ya Uviko-19, Mkoa wa Dodoma ulipata madarasa 776 pamoja na samani zake. Tunampongeza Rais wetu na serikali yake” alisema Dkt. Mganga.
Akiongelea lengo la hafla hiyo, alisema kuwa ni nia njema ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwatambua, kuwathamini na kuwapongeza walimu, wazazi na wadau wa elimu kwa kuongeza ufaulu katika mitihani.
Alisema kuwa matarajio ya Mkoa wa Dodoma ni kuingia katika nafasi tano za mwanzo. “Kupitia tuzo hizi, zitachangia katika kutoa hamasa kwa walimu na wanafunzi kufanya vizuri zaidi” alisema Dkt. Mganga.
Akiongelea tuzo hizo, alizitaja kuwa ni tuzo kwa shule za msingi za serikali zilizofaulisha kwa daraja A kwa masomo yote sita. Tuzo kwa shule za sekondari zilizofaulisha kwa daraja la I kwa pointi saba. Nyingine ni tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari za serikali waliofaulu kwa daraja I pointi saba kwa wavulana na pointi saba hadi tisa kwa wasichana. “Tuzo ya nne ni walimu wa shule za sekondari za serikali waliofaulisha kwa daraja A kwa mtihani wa kidato cha Nne” alisema Dkt. Mganga.
Akiongelea waliofanikisha halfa hiyo, alimtaja Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuwa mstari wa mbele. “Napenda kutoa shukurani kwa wadau kuwezesha tukio hili. Kipekee nitoe shukrani sana kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru. Shughuli hii ilikuwa tuifanyie katika uwanja wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kwa tahadhari ya mvua, nikamshirikisha Mkurugenzi wa Jiji nae kufadhili ukumbi huu” alisema Dkt. Mganga kwa sauti ya shukrani.
Mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga alipokuwa akitoa neno kuhusu tuzo za taaluma Mkoa wa Dodoma katika hafla ya utoaji tuzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha Nne mwaka 2021 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.