UANDIKISHAJI wa orodha ya wapigakura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umevunja rekodi baada ya zaidi ya watu milioni 19.7 ambayo ni sawa ya asilimia 86 ya malengo yaliyowekwa kujitokeza kujiandikisha huku mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kinara kwa kuandikisha kwa asilimia 108.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ilikadiria kuandikisha Wapigakura 22,916,412 ambao ni sawa na asilimia 85 ya Wananchi wenye sifa za kupigakura ambao kati hao Wanaume 10,924,479 na Wanawake 11,991,933.
Kutokana na kufanya vizuri kwa Mikoa yote, wakuu wa Mikoa na Wilaya kumemfanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo kusitisha maamuzi yake ya kupeleka Dokezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli la kuchukuliwa hatua za kinidhamu endapo wangeshindwa kuhamasisha na wangeandikisha chini ya asilimia 50.
Akitoa tathimini ya siku 10 za uandikishaji wapigakura, Jafo alisema wapigakura 19,681,259 wameandikisha ambayo ni sawa na asilimia 86 ya lengo la kuandikisha wapigakura 22,916,412.
Jafo alisema hadi kufika Oktoba 17 mwaka huu, wapigakura zaidi ya milioni 19.68 wamejiandikisha wanaume wakiwa ni 9,529,990 na wanawake ni 10,151,267 ambao ni sawa na asilimia 86 ya lengo la kuandikisha wapigakura zaidi ya milioni 22.9.
Uandikishaji wa mwaka huu umekuwa na mafanikio ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2014 ambapo walioandikishwa walikuwa ni 11,882,086 ambayo ilikuwa ni asilimia 63 ya makadirio ya kuandikisha wapigakura 18,787,820.
Waziri Jafo alibainisha changamoto zilizojitokezwa wakati wa zoezi la uandikishaji kuwa ni hali ya mvua katika baadhi ya maeneo pamoja na ile ya wananchi kuchanganya na zoezi la uboreshaji wa Dafari la Kudumu la wapiga kura na baadhi ya vituo kuwa mbali na kuwa vigumu kufikiwa na wananchi.
Alifafanua kuwa kutokana na changamoto hizo siku za uandikishaji ziliongezwa kutoka siku saba mpaka kufukia siku kumi hivyo zoezi hilo lilifanyika kuanzia Tarehe 7 – 17/10/2019.
Akizungumzia takwimu za uandikishaji wapigakura kimkoa, Jafo alisema jumla ya mikoa 26 imeshiriki katika zoezi la uandikishaji ambapo Dar es Salaam ulishika nafasi ya kwanza kwa kuandikisha wapigakura 2,892,535 ambayo ni asilimia 108.
Alisema Dar es Salaam imefuatiwa na Mkoa wa Pwani ulioandikisha 568,627 (asilimia 96), Mwanza iliyoandikisha 1,340,177 sawa na asilimia 95, Tanga iliyoandikisha 983,104, Singida iliyoandikisha 610,344 ikiwa ni kwa asilimia 90 kila mmoja na Morogoro iliandikisha 1,075,379 sawa na asilimia 89.
Mikoa mingine ikionyesha na idadi ya wapiga kura ni Mbeya 776,811 (asilimia 83), Ruvuma 651,257 (asilimia 88), Katavi 243,163 sawa na asilimia 88. Mtwara 604,670 (asilimia 86), Dodoma 893,890 (asilimia 85), Rukwa 410.760 (asilimia 85) na Arusha 787,232 (asilimia 85).
Mikoa mingine ni Lindi iliyoandikisha 396,832 (asilimia 84), Iringa 433,259 (asilimia 84), Mara 673,065 (asilimia 80), Kilimanjaro 741,130 (asilimia 79), Geita 664,100 (asilimia 79), Manyara 565,827 (asilimia 78), Tabora 876,664 (asilimia 78), Songwe 402,840 (asilimia 78), Kagera 961,520 (asilimia 78), Shinyanga 583, 928 (asilimia 76), Simiyu 568,342 (asilimia 76), Njombe 290,791 (asilimia 75) na Kigoma 676,012 (asilimia 65).
Sambamba na hili, Jafo alitoa cheti na kombe kwa mikoa na halmashauri zilizofanya vizuri katika uandikishaji wa wapigakura wa uchanguzi wa serikali za mitaa.
Jafo alitaja mikoa iliyofanya vizuri na iliyopewa kombe na mingine cheti kuwa ni pamoja na Dar es Salaam iliyoandikisha kwa asilimia 108, Pwani kwa asilimia 96, Mwanza kwa asilimia 95, Tanga kwa asilimia 90, Singida kwa asilimia 90.
Kwa upande wa Halmashauri Jafo alizitaja na kuzitunukia Halmashauri tano ambazo ni Mlele DC iliyoandikisha wapigakura 27,196 (asilimia 152), Ngorongoro DC iliyoandikisha 96,622(asilimia 129), Kibiti DC iliyoandikisha 60,539 (asilimia 126), Temeke iliyoandikisha 879,619 (asilimia 122) na Monduli iliyoandikisha 91,363(asilimia 122).
Wakati huo huo Jafo alitaja Halmashauri 5 zimefanya vizuri kuandikisha waandishi wengi zaidi kuwa ni Temeke ambao wameindikisha wapigakura 879,619 (asilimia 122), Ilala iliyoandikisha wapigakura 820,600 (asilimia 111) manispaa ya Mwanza iliyoandikisha 224,901(asilimia 105), Ubungo MC imeandikisha 542,728 (asilimia 103) na Kinondoni iliyoandikisha 569,872 (asilimia 96).
Aidha, Jafo ametumia fursa hiyo kutaka hamasa iliyotumika kushawishi wananchi kujiandikisha ndiyo itumike wakati wa kupiga kura.
“Ni imani yangu watu wengi pia watajitokeza wakati wa kupiga kura ya kuwachangua viongozi ambao ndio msingi wa maendeleo ya wananchi,” alisema.
Jafo amewataka watanzania kuendeleza amani na utulivu wakati wa kuchukua fomu, kurudisha fomu na kupiga kura huku akisisitiza kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa wagombea na wapigakura.
Vilevile, Jafo amewashukuru viongozi wote waliojitokeza kujiandikisha kwenye Orodha ya Daftari la Wapigakura kuanzia gazi za Taifa, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na vitongoji na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi hatimaye kufanikisha zoezi hili.
Uchaguzi wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu na utafanyika katika vijiji 12, 319, mitaa 4,264 na vitongoji 64, 384
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.