Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea kudhihirisha ubora wake kuwa siyo kwenye kukusanya mapato ghafi tu bali hata katika mchezo wa soka ambapo timu yake ya Dodoma Jiji FC imetwaa ubingwa wa ligi daraja la kwanza kwa msimu huu wa 2019/2020.
Hayo yamedhihirika baada ya timu hiyo kufanya vizuri katika Ligi ya Daraja la Kwanza kwa kuongoza kundi A na kupanda Daraja kuingia Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kubwa likiwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuifunga kinara wa kundi B timu ya Gwambina FC ya Misungwi Mwanza goli 1-0 na kutawazwa mabingwa.
Aidha, timu hiyo imezoa zawadi ya kocha bora wa msimu ambaye ni Mbwana Makata na mfungaji bora ambaye ni mshambuliaji wake Anuary Jabir.
Akizungumza baada ya mchezo wa kumsaka bingwa wa ligi hiyo uliofanyika katika uwanja wa Chamazi Jijini Dar es salaam kocha mkuu wa timu ya Dodoma Jiji Mbwana Makata amewapongeza wachezaji wa timu yake kwa kupambana kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa ligi lakini zaidi kwa kushinda taji la bingwa wa jumla wa michuano hiyo.
Makata alisema kuwa licha ya changamoto nyingi walizokutana nazo na ugumu wa kundi A, lakini wachezaji walionesha kujiamini na kusikiliza maelekezo aliyokua anayatoa kitu kilichopelekea ushindi na kuongeza kuwa, lengo lao sasa lipo kwenye Ligi Kuu huku akiwatoa hofu mashabiki kuwa watafanya vizuri.
“Niwashukuru Bodi ya Ligi kwa kuendesha ligi vizuri, nimshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, wakuu wa idara na wafanyakazi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma waliojitoa kwa ajili ya timu, wadau wa michezo pamoja na mashabiki wetu kwasababu bila wao tusingekabidhiwa kombe leo, niwaahidi kuwa tunakwenda kupambana na kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu” Aliongeza Makata.
Kwa upande wake msemaji wa timu hiyo Ramadhani Juma amewashukuru Azam Media Group kwa kuonesha mchezo wa fainali hizo mubashara kwani kumewafanya watu kuona ubora wa timu ya Dodoma Jiji na kuondoa makandokando yaliyokuwa yanasemwa kuwa timu hiyo ilikua ikibebwa.
“Kila kitu kilikua wazi kabisa, maneno yalikuwa mengi kuwa tunabebwa, lakini baada ya mchezo wa fainali simu zilikua nyingi kutoka kwa watazamaji kuwa timu yetu imesakata kabumbu safi, na niwahakikishie wana Dodoma kuwa tuna timu nzuri sana kwani tuliwazidi Gwambina kwa kila kitu, tulikua na uwezo wa kufunga zaidi ya goli tatu lakini ndiyo mchezo wa soka ulivyo, hivyo tukutane Ligi Kuu, mazuri yanakuja” alisema Ramadhani.
Naye mfungaji wa goli la ushindi la Dodoma Jiji FC ambaye ndiye kinara wa magoli wa ligi hiyo Anuary Jabir alisema kuwa bado ana deni kwa mashabiki wa timu hiyo la kufanya vizuri katika michuano mikubwa ya Ligi Kuu, huku akimshukuru mwalimu wake, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzake kwa ushirikiano waliompa hadi akafanikiwa kuwa mfungaji bora kwa kuweka wavuni mabao 11 katika msimu mzima.
Kikosi cha timu ya Dodoma Jiji FC kilichofanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza 2019/20 baada ya kuifunga timu ya Gwambina FC goli 1 - 0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es Salaam.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.