KITUO cha Afya Mkonze kimefanikiwa kuongeza utoaji huduma kwa wananchi kufuatia Serikali kujenga majengo matano na kuwaondolea adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze, Dkt. Twilumba Lihweuli alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa majengo matano katika kituo hicho kwa kamati ya siasa ya Wilaya ya Dodoma mjini.
Dkt. Lihweuli alisema kuwa ujenzi wa majengo mapya matano umegharimu shilingi 400,000,000 zilizotoka Serikali kuu. Aidha, “Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliongeza shilingi 287,826,442 ikiwa ni gharama kwa ajili ya kufunga mfumo Madhubuti wa Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, kujenga njia za watembea kwa miguu zinazounganisha majengo, kununua vifaa mbalimbali vya kumalizia ujenzi katika majengo yote matano, pia ilihusisha gharama za kuweka mfumo wa maji taka, malipo ya mafundi ujenzi, ufungaji wa mfumo wa umeme - TANESCO, kazi za ziada na ujenzi wa ‘Incinerator’” alisema Dkt. Lihweuli.
Akiongelea malengo ya ujenzi huo, mganga mfawidhi huyo alisema kuwa kuongeza majengo katika kituo hicho na ukarabati wa majengo ya zamani imesaidia kuboresha huduma kwa ujumla na pia kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa watumishi. “Lengo hilo limetimia kwa asilimia mia moja. Majengo yameongezeka kutoka majengo mawili hadi kufikia majengo saba, ukarabati wa majengo ya zamani umefanyika hivyo kufanya mazingira ya kutolea huduma ndani na nje yawe mazuri na muonekano mzuri wenye kuvutia wateja” aliongeza Mganga Mfawidhi.
Akizungumzia mafanikio ya mradi, mganga huyo aliyataja kuwa ni utoaji wa huduma za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito unafanyika kwa ufanisi. “Mpaka sasa jumla ya wazazi 25 wamejifungulia kwenye jengo jipya la kujifungulia. Pia wagonjwa 325 wameshahudumiwa katika jengo jipya la maabara tokea lianze kutumika” alisema Dkt. Lihweuli.
Mganga huyo aliyataja majengo matano yaliyojengwa katika kituo cha Afya Mkonze kuwa ni jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti (mochuari) na nyumba ya mtumishi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma mjini, Elirehema Nassari aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ujenzi na ukarabati wa kisasa katika kituo cha Afya Mkonze. Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kwa kutoa fedha za nyongeza kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Vilevile, alimpongeza Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo Ludigija Ndatwa kwa kusimamia vizuri ujenzi huo na kukabiliana na changamoto ya maji iliyokuwa ikilikabili eneo hilo.
Kituo cha Afya Mkonze kilianzishwa mwaka 1993 kikiwa ni moja ya vituo vinne vya Afya vya Serikali vilivyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma mjini Elirehema Nassari (kulia) akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Shabani Juma walipotembelea Kituo cha Afya Mkonze kujionea kazi ya uboreshaji wa Kituo cha Afya Mkonze.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma mjini Elirehema Nassari akongea na watumishi pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ya Dodoma mjini walipotembelea kituo cha Afya Mkonze.
Jengo la wadi ya wazazi na watoto katika kituo cha Afya Mkonze lililojengwa kwa fedha kutoka Seriakali kuu.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma mjini baada ya kukagua jengo jipya la Upasuaji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Daktari Joseph Mdachi (mwenye sweta jekundu) na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze Daktari Twilumba Lihweuli wakisikiliza maelekezo kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma mjini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.