Na. Valeria Adam, DODOMA
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza rasmi ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024, ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alitoa tangazo la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo alieleza kuwa tangazo hilo limetolewa chini ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2024 pamoja na matangazo ya Serikali namba 571, 572, 573 na 574 ya mwaka 2024.
"Mtiririko wa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni utangulizi, masharti muhimu ya uchaguzi na ratiba ya uchaguzi. Kwa wagombea wa nafasi za uongozi, wanatakiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu. Uteuzi wa wagombea utafanyika siku 19 kabla ya uchaguzi na endapo kutakuwa na mgombea mmoja pekee kwa nafasi husika, atateuliwa moja kwa moja” alisema Mchengerwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Juma Ally Khatib alisema kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Kadhalika ameonya kuwa uchaguzi usisababishe amani ya nchi kuvurugika. "Vyama vya siasa vipo tayari kwa uchaguzi na uchaguzi huu utatoa tafsiri ya uchaguzi ujao” alisema Khatib.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake. Mojawapo ya madhumuni ya kuwepo kwa serikali za mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.